MABOSI wa Yanga, wamefuta mipango ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Uganda ‘The Craenes’ na Klabu ya KCCA ya nchini Uganda, Allan Okello baada ya kufanikiwa kuipata saini ya winga wa TP Mazembe, Phillipe Kinzumbi.
Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, Yanga imefuta mipango ya kumsajili Okello mara baada ya kufanikisha dili la Kinzumbi ambaye mwenyewe ameonesha nia kubwa kuhitaji kuichezea timu hiyo.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ndiye aliyehusika kufanikisha usajili wa Kinzumbi baada ya kuwashawishi viongozi wamsajili katika kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.
Aliongeza kuwa, usajili wa Kinzumbi huenda ukamuondoa mmoja wa mawinga wa timu hiyo, Mghana Bernard Morrison ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu au Tuisila Kisinda aliyekuwepo kwa mkopo akitokea RS Berkane ya Morocco.
“Awali uongozi ulikuwepo katika mipango mikubwa ya kuipata saini ya Okello tangu usajili wa dirisha dogo msimu huu, lakini ilishindikana kutokana na sababu ya kiuongozi.
“Sababu hizo zikasogeza mipango yake ya usajili katika dirisha kubwa la msimu ujao, lakini mipango hiyo haitakuwepo tena mara baada ya kumpata Kinzumbi.
“Usajili wa Kinzumbi ni mapendekezo ya Kocha Nabi ambaye mwenyewe amewaambia viongozi anamtaka staa huyo wa TP Mazembe ambaye katika mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Mkapa, alionekana kuwasumbua mabeki wetu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alizungumzia hilo la usajili na kusema kuwa: “Yanga hakuna mchezaji tutakayemuhitaji, halafu tukamkosa. Kama uongozi tupo tayari kutumia gharama zote katika usajili ili kumpata mchezaji anayehitajika na benchi letu la ufundi.”
0 Comments