Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrrey Mwanri
Kwa ufupi
Katika tukio la Nzega lilitokea Julai 26, kwenye Kijiji cha Uchama wilayani Nzega, watu watano walifariki dunia baada ya kucharazwa bakora kisha kuchomwa moto na watu waliosadikiwa kuwa ni Sungusungu.
By Daniel Makaka, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Ikiwa ni takriban miezi miwili tangu watu wanaodaiwa kuwa walinzi wa jadi maarufu Sungusungu kuwacharaza viboko watu watano na kuwasababishia vifo kwa imani za kishirikina, tukio kama hilo la ucharazaji bakora limeibukia wilayani Sengerema.
Katika tukio la Nzega lilitokea Julai 26, kwenye Kijiji cha Uchama wilayani Nzega, watu watano walifariki dunia baada ya kucharazwa bakora kisha kuchomwa moto na watu waliosadikiwa kuwa ni Sungusungu.
Kufuatia mauaji hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrrey Mwanri alizitaka kamati za ulinzi na usalama ngazi ya mkoa na ile ya Wilaya ya Nzega kusitisha shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na Sungusungu katika kijiji hicho.
Mwanri alisema amechukua hatua hiyo baada ya Sungusungu hao kutekeleza mauaji hayo ya watu watano ambao wote ni wanawake wakiwatuhumu kuwa washirikina.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa alisema wakati wakiendelea na upelelezi wa tukio hilo watu kadhaa walikuwa mikononi mwa jeshi hilo ili kuweza kubaini waliotekeleza mauaji hayo.
Wakazi wa Kijiji cha Nugonya, Kata ya Nyamazugo wilayani Sengerema nao wamewalalamikia Sungusungu kuwacharaza viboko na kuwafukuza katika eneo wanaloishi pasipo na sababu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walilaumu kitendo hicho ambacho walidai ni cha kikatili.
“Tunajua kazi mojawapo ya Sungusungu ni kukamata wahalifu na kuwafikisha kwenye mamlaka husika, lakini suala la kutuchapa viboko ni la uonevu na linatakiwa kuchukuliwa hatua,” alisema Juma Kalamu
Alisema Serikali inapaswa kuwawekea mwongozo wautendaji kazi Sungusungu.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Joseph Senyenge aliahidi kufuatilia suala hilo na kuahidi kuwa wataobainika hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.
Mwenyekiti wa ulizi wa kijiji hicho, Elias Kisununa alisema atafanya uchunguzi ili kubaini watu wanaofanya vitendo hivyo.
Msaidizi wa kisheria wilayani Sengerema, James Sendama alilaani tukio hilo kwa kuwa kuwachapa viboko wananchi ni kinyume na haki za binadamu.
MWANANCHI
MWANANCHI
0 Comments