LONDON, ENGLAND. MASTAA wa Ligi Kuu England wameendelea kuchuma pesa kwa mishahara mikubwa. Wapo wanaoitendea haki mishahara yao, lakini wapo pia wasiotendea haki mishahara hiyo. Wafuatao ni mastaa 10 wanaolipwa zaidi kwa kila dakika wanayocheza.
David De Gea (Pauni 2,567.90)
Kipa huyu wa kimataifa wa Hispania, ni mmoja kati ya wachezaji waliocheza dakika nyingi msimu uliopita. Alicheza dakika 4,050 na kwa mshahara wake wa Pauni 10,400,000 kwa msimu, basi United ilikuwa imemlipa De Gea Pauni 2,567.90 kwa kila dakika aliyocheza.
Raheem Sterling (Pauni 2,580.65)
Winga wa kimataifa wa England. Mshahara wake kwa msimu pale kwa matajiri wa Kiarabu ni Pauni 9,360,000 kwa mwaka. Msimu uliopita alicheza kwa dakika 3,627 hivyo ukigawanya mshahara wake wa Pauni 9,360,000 kwa dakika hizo, ni wazi Man City ilimlipa Sterling kiasi cha Pauni 2,580 kwa kila dakika ambayo alivaa jezi yao.
David Silva (Pauni 2,852)
Kiungo mahiri mchezeshaji wa Kihispaniola ambaye dakika zake alizocheza pale Manchester City hazitofautiani sana na dakika za Sterling. David Silva alicheza dakika 3,646 na kwa dakika alilipwa Pauni 2,852.
Hii ni kwa mujibu wa mshahara wake wa Pauni 10,400,000 anaolipwa na matajiri hao wa Kiarabu pale Etihad.
Zlatan Ibrahimovic (Pauni 3,379.26)
Kama si kuumia katika pambano la michuano ya Europa dhidi ya Anderlecht, si ajabu Zlatan angekuwa amecheza dakika nyingi zaidi za soka msimu uliopita.
Zlatan ambaye alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliolipwa zaidi msimu huo, alicheza dakika 3,847 na kwa kila dakika, United ilijikuta inamlipa kiasi cha Pauni 3,379.26. Mshahara wake wa msimu ulikuwa Pauni 13,000,000.
Eden Hazard (3,391.64)
Mchezaji staa zaidi Chelsea kwa sasa huku akiwa mmoja kati ya wachezaji wanaolipwa zaidi kikosini hapo. Kwa jumla Hazard analipwa Pauni 11,440,000 kwa mwaka na tajiri wake, Roman Abramovich.
Msimu uliopita, Hazard, alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliolipwa pesa nyingi zaidi kwa kila dakika aliyokuwa uwanjani. Kwa kila dakika alilipwa kiasi cha Pauni 3,391. Hiyo ni kwa dakika 3,373 alizocheza msimu huo.
Paul Pogba (Pauni 3,466.67)
Ulikuwa ni msimu wake ambao alicheza akiwa mwanasoka ghali zaidi duniani baada ya United kulipa dau la Pauni 89 milioni kumnasa kutoka Juventus. Pogba alikuwa mmoja kati ya wachezaji wa United waliokuwa wanalipwa zaidi Old Trafford.
Msimu uliopita alicheza kwa dakika 4,350 ambazo kwa pato lake la mwaka la Pauni 15,080,000 linaifanya United iwe imemlipa kiasi cha Pauni 3,466 kwa kila dakika aliyogusa uwanjani msimu uliopita.
Sergio Aguero (£3,562.66)
Haukuwa msimu mzuri kwa Aguero baada ya kuwasili kwa kocha, Pep Guardiola, pale Man City ambaye nyakati kadhaa alimwacha nje. Aguero alicheza kwa dakika chache tu Ligi Kuu England kuliko wakati mwingine wowote tangu awasili klabuni hapo mwaka 2011.
Alicheza dakika 3,503 msimu uliopita na kwa pato lake la mshahara wa Pauni 12,480,000 basi Aguero alijikuta akilipwa kiasi cha Pauni 3,562 kwa kila dakika aliyocheza akiwa na jezi ya City.
Cesc Fabregas (4,528.69)
Haukuwa msimu mzuri kwa Cesc Fabregas licha ya Chelsea kutwaa ubingwa. Kocha Antonio Conte alikuwa akimsugulisha benchi mara nyingi kiasi cha kuhusishwa kuondoka Stamford Bridge.
Fabregas alicheza kwa dakika chache, lakini ambazo zilimfanya alipwe kiasi kikubwa kwa dakika kuliko baadhi ya mastaa kama akina Pogba, Silva, Zlatan na wengineo. Alicheza dakika 1,952 tu msimu uliopita, lakini kwa pato lake la Pauni 8,840,000 alijikuta akilipwa kiasi cha Pauni 4,528.69 kwa kila dakika ambayo alicheza msimu uliopita.
Yaya Toure ( £4,990.00)
Kama ilivyokuwa kwa Cesc Fabregas, msimu uliopita haukuwa mzuri kwa kiungo huyo wa kimataifa wa Ivory Coast. Alianza kusugua benchi katika kikosi cha Kocha Pep Guardiola, baada ya kocha huyo kukorofishana na wakala wa Toure, Dimitr Seluk. Toure alianza kucheza Desemba na hadi kufikia mwishoni mwa msimu alikuwa amecheza dakika 2,501 za soka. Akiwa ni mmoja kati ya mastaa wanaolipwa sana Manchester City na England huku akiondoka na bunda la Pauni 12,480,000 kwa mwaka, Toure alijikuta akilipwa kiasi cha Pauni 4,990.00 kwa kila dakika aliyotinga uwanjani na jezi ya City.
Wayne Rooney (5,598.34)
Ulikuwa ni msimu wa mwisho kwa Wayne Rooney pale Old Trafford baada ya misimu 13. Aliondoka klabuni hapo akiwa mchezaji anayelipwa zaidi klabuni. Mshahara wake ulikuwa Pauni 13, 520,000 kwa mwaka. Hata hivyo, ulikuwa ni msimu ambao Rooney alicheza dakika chache zaidi kulinganisha misimu yote ya nyuma aliyokipiga Trafford. Rooney alijikuta akicheza kwa dakika 2,415 tu na kwa kufanya hivyo alikuwa akilipwa Pauni 5,598.34 kwa kila dakika aliyoingia uwanjani na jezi ya United. Kwa kifupi ndiye mchezaji aliyelipwa pesa nyingi zaidi kwa dakika katika msimu uliopita akimuacha Yaya Toure.
0 Comments