Mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Kalangalala, mjini Geita, amefariki dunia baada ya kunajisiwa na mtu asiyejulikana nyumbani kwao, usiku wa kuamkia juzi.
Tukio hilo ni mwendelezo wa vitendo vya ukatili, mateso na udhalilishaji dhidi ya watoto ulio kinyume na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, inayoeleza kwamba mtoto anapaswa kulindwa na kuthaminiwa.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo alikiri kutokea kwa tukio hilo akieleza kwamba mtu mmoja anashikiliwa na upelelezi unaendelea.
Inadaiwa kwamba, tukio la kunajisiwa kwa mwanafunzi huyo lilitokea saa 8:00 usiku wa kuamkia juzi, baada ya mtuhumiwa kugonga mlango alimokuwa amelala mtoto huyo akiwa peke yake.
Inaelezwa mama wa mwanafunzi huyo, Pegi Kevline aliondoka nyumbani tangu juzi jioni kwenda kazini, aliporejea saa 2:00 asubuhi, siku iliyofuata alikuta majirani wakiwa wamekusanyika nyumbani kwake.
Habari zinasema, kabla ya kufanya unyama huyo, mbakaji alifika na kugonga mlango katika nyumba hiyo na mtoto huyo alifungua mlango akidhani ni mama yake, kumbe alikuwa mwanamume huyo, aliyeingia na kabla ya kufanya ukatili huo alimziba mdomo kwa khanga ili asipige kelele, kisha kuanza kumnajisi hadi kufa.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Mtaa wa Nyerere na kwamba wakati likitokea, kuna mtu alifika nyumbani kwa mmoja wa wapangaji na kugonga mlango, lakini mpangaji huyo alipiga kelele na huyo mtu kukimbia.
Konyo alisema kwamba baada ya mtu huyo kukimbia, wapangaji walitoka nje na kuona mlango wa chumba alimokuwa amelala mtoto huyo ukiwa wazi, ndipo walichungulia ndani na kuona mtoto huyo amelala kitandani, akiwa amefungwa nguo mdomoni.
Kamanda Konyo alibainisha kwamba mtu mmoja anayedaiwa kuwa na mazoea na familia hiyo anashikiliwa kusaidia upelelezi, hata hivyo hakutaka kumtaja jina kuepusha kuvuruga upelelezi.
Mwenyekiti wa mtaa anena
Mwenyekiti wa mtaa huo, Dua Kaburi alisema kuwa baada ya tukio hilo, mtuhumiwa aliingia chumba kingine cha Aneth Nyamhanga akidhaniwa pia kutaka kubaka, lakini alipigiwa kelele na kukimbia.
“Mbakaji huyo alikwenda pale mapema jioni akataka kumbaka shemeji yake ambaye naye ni mpangaji, akapigiwa simu kaka yake, alipofika alimpiga mtuhumiwa akaondoka huku akisema lazima awabake wote watatu akiwamo mtoto huyo ili awaambukize Virusi Vya Ukimwi,” alisema Kaburi.
Alisema kuwa tukio hilo linatokana na baadhi ya watu kukaribisha watu wasiowafahamu na kwamba, kwenye nyumba hiyo yenye wapangaji 10 ni wawili waliojiorodhesha kwenye kitabu cha mtaa.
“Nimewapa siku mbili kuanzia leo (jana) wawe wamejiandikisha, vinginevyo tutawakamata na kuwapeleka kwenye vyombo husika,” alisema Kaburi.
0 Comments