Header Ads Widget

Siku 100 Za Rais Magufuli Ikulu




Ni kweli siku hazigandi kwamba Rais John Magufuli aliyeingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, ametimiza siku 100 leo.

Tangu alipotoa hotuba yake siku ya kuapishwa na ile ya uzinduzi wa Bunge la 11, Rais Magufuli amejitahidi kuishi katika maneno yake kwa kutenda kile anachokisema.


Miongoni mwa mambo aliyoahidi ni kupambana na rushwa pamoja janga la dawa za kulevya, akisema dawa za kulevya zimeathiri vijana wengi, hivyo akaahidi kushughulikia mtandao huo na wakubwa wanaohusika.


Kwa upande wa rushwa, Rais Magufuli aliahidi kupambana na ufisadi na rushwa na katika kutekeleza hilo, alisema ataunda mahakama maalumu ya kushughulikia wezi wakubwa yaani mafisadi.


Pia aliahidi kuwashughulikia wafanyakazi wazembe ili Serikali yake isiendelee kulea watu wanaolipwa mishahara tu wakati hawafanyi kazi yoyote.


Katika kubana matumizi ya serikali, aliahidi kudhibiti warsha ambazo hazina umuhimu katika Serikali wala kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi.


Aliahidi pia kudhibiti safari za nje, ambazo zimekuwa zikigharimu Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.


Rais Magufuli pia alisema Serikali yake itaongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato, ukizingatia kuwa kodi ni kitu muhimu na ni lazima zikusanywe.


Aliahidi kufufua viwanda viliyobinafsishwa, ambavyo baadhi alidai vimegeuzwa mazizi ya mbuzi wakati waliopewa kwa madhumuni ya kuviendeleza.


Aliahidi pia kushughulika na kero zinazolalamikiwa kutendwa na polisi, hospitali, mizani, Mahakama, maliasili na vilio vya wachimbaji.

Tayari Rais Magufuli ametenda yale ambayo aliyaahidi kwa Watanzania. Amebana matumizi ya serikali kwa kudhibiti safari zisizo na tija, matumizi yasiyo ya lazima, ameshughulikia watumishi wazembe, ameshughulikia mafisadi ndani ya serikali na kutoa elimu ya bure.


Alivyoanza kazi
Mara tu baada ya kuingia ofisini, alimuapisha Mwanasheria Mkuu, George Masaju aliyemteua muda mfupi tu baada ya kuapishwa.


Katika siku zake hizo za mwanzo, alitumia mtindo wa kufanya ziara za kushtukiza katika taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na kukemea viongozi wazembe na wanaoendekeza ufisadi na rushwa serikalini.

Mtindo wake huo, ukatumiwa pia na watendaji wengine wa Serikali wakiwamo mawaziri na wakuu wa mikoa na wengine.

Katika siku zake hizo za mwanzo, Rais Magufuli pia alifanya mabadiliko makubwa Ikulu kwa kufuta baadhi ya vitengo, kikiwamo cha lishe na benchi la wageni na kuagiza wananchi wote wenye matatizo waanzie ngazi za chini.

Atoa Msimamo wake
Novemba 7, mwaka jana akiwa Ikulu, Dar es Salaam, alikutana na watumishi wa Serikali ikiwa ni pamoja na manaibu katibu wakuu, manaibu wakuu na watendaji wakuu wa Serikali.

Katika kikao hicho, aliwataka kujiandaa kufanya kazi kwa ufanisi katika Serikali ya awamu ya tano chini yake. huku akiwasisitiza juu ya dhamira yake ya kuendeleza kaulimbiu yake ya “Hapa kazi tu”.

Kikao hicho pia kiliudhuriwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade ambapo alitoa mwelekeo wa Serikali anayoitaka.

Afuta Safari za Nje
Rais Magufuli alitumia kikao hicho kutangaza kufuta safari zote za nje ya nchi hadi hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine, na kueleza shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi.

Alisema mtumishi atasafiri nje iwapo kutatokea jambo la dharura, na lazima kibali kitolewe na yeye, Katibu Mkuu Kiongozi au Makamu wa Rais.

Badala yake aliwataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi.

Hadi sasa, Rais Magufuli bado hajakwenda safari yoyote ya nje ya nchi zaidi ya kuwatuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenda kumwakilisha kwenye shughuli mbili tofauti.

Safari zake ndani ya nchi
Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alisafiri kwa mara ya kwanza nje ya Dar es Salaam alipokwenda mkoani Dodoma ambako alifungua Bunge la 11.

Katika mkutano wake, Rais Magufuli alijikuta akisusiwa hotuba yake na wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga uteuzi wake na kutomtambua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kama rais halali, baada ya kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Januari 12, mwaka huu, Rais Magufuli alisafiri kwa ndege ya kukodi kwenda Zanzibar ambako alihudhuria maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Januari 21, mwaka huu alifanya ziara ya kwanza mkoani Arusha, ambako alikwenda pia katika Chuo cha Maofisa wa Kijeshi (TMA) Monduli kutunuku vyeo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuhitimu mafunzo, huku naye akiwa amevalia sare za jeshi hilo.

Februari 5, mwaka huu pia Rais Magufuli alisafiri kwa gari kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Singida kuhudhuria maadhimisho ya miaka 39 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Akataa sherehe ya kifahari Bungeni
Rais alionekana tofauti na viongozi wengine waliomtangulia baada ya kuifanya sherehe ya kuzindua Bunge kutokuwa ya kifahari na hivyo akaokoa Sh milioni 251, ambazo aliagiza zikanunue vitanda Hospitali ya Taifa Muhimbili.


Jumla ya vitanda 300, magodoro 300, viti maalumu vya wagonjwa 30, vitanda vya kubeba wagonjwa 30 na mashuka 1,695.


Afuta gwaride la Uhuru
Novemba 9, mwaka jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alitangaza kuwa Rais Magufuli aliamua kufuta shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru na kwamba fedha zitakazookolewa atazipeleka sehemu nyingine.


Fedha Sh bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharimia shamrashamra za Siku ya Uhuru, ambazo zingefanyika tarehe 9 Desemba 2015, Rais aliamuru zitumike kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3.

Baraza la Mawaziri
Desemba 10, mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri ambalo alianza kwa kuteua mawaziri 19, ingawa wizara ni 18. Mawaziri sita kati ya hao ni wanawake.

Katika uteuzi wake, aliacha wazi nafasi nne za uwaziri kwa madai alikuwa akitafuta watu watakaofaa kuteuliwa kuongoza wizara husika.

Wizara ambazo hakuteua mawaziri katika baraza lake la awali alilolitangaza ni Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Desemba 23, mwaka jana ikiwa ni siku 13 tangu alipotangaza Baraza la Mawaziri, Rais Magufuli alikamilisha baraza lake kwa kuwataja mawaziri wanne waliokuwa wamebakia.

Uteuzi wa Rais Magufuli umekuwa wa tofauti ambapo viongozi wengi aliowateua kushika nafasi mbalimbali ni wasomi wa ngazi ya uprofesa na udaktari.

Post a Comment

0 Comments