
Nesi wa kituo cha afya cha Katoro wilaya Geita mkoani Geita, Leah Mganga( 33) mkazi wa katoro, anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za mauaji ya kichanga.
Tukio hilo la kushangaza limetokea jana majira ya saa tisa usiku, wakati mama mmoja aitwaye Mariam Gekera (23) mkazi wa Nyarugusu, alipofikishwa katika kituo hicho kwa ajili kujifungua na kisha kupokelewa na nesi huyo ambaye alikuwa zamu kwa ajili ya kumhudumia.
Akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo huku akibubujikwa na machozi mzazi huyo alisema kuwa pamoja na kupokelewa na nesi huyo na kupimwa na kuambiwa mimba imefikia kuzaliwa lakini huduma za kumsaidia ili ajifungue salama zilianza kusuasua .
Mama huyo alisema alifanikiwa kujifungua japo kwa shida yeye mwenyewe mtoto akiwa mzima na analia, lakini kwa bahati mbaya damu zilimrukia nesi huyo kitendo ambacho kilimkera nesi na kuanza kutoa matusi kwa mzazi huyo.
Kufuatia hali hiyo nesi alikwenda kubadilisha vazi na kurudi na kubeba kichanga na kuondoka nacho huku mzazi akiuliza mtoto anapelekwa wapi.
“Muda mfupi nesi alirudi akiwa amekibeba kichanga hicho kwa mikono miwili na kusema “kichanga chako ni kilo tatu na ni kivulana lakini kimekufa”.alisema mama huyo
Kufuatia tukio hilo malunde1 blog haikukaa kimya,iliamua kumfuata nesi Leah Mganga ili kujua kulikoni lakini alisema taarifa zilizotolewa na mzazi huyo si za kweli na kuongeza kuwa yeye alitoa msaada kama kawaida na baada ya kurukiwa alikwenda kubadilisha vazi jingine na aliporudi alikuta kichanga kimekufa.
Mganga mfawidhi wa kituo hicho Dk. Alex Bundala alikiri kuwepo kwa tukio hilo kwenye kikao cha wajumbe wa serikali ya kijji walichokuwa wamekiitisha mapema asubuhi ya leo kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Joel Mazemle pamoja na uongozi wake wamelaani kitendo kilichofanywa na nesi na kuiomba serikali kuchukua hatua kali dhidi ya mtuhumiwa huyo kwani ni vitendo vingi viovu vinavyofanywa na manesi hao katika kituo hicho.
Jeshi la polisi mkoani Geita limethibitisha kutokea kwa tukio na kusema mtuhumiwa anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.
Na Valence Robert-Malunde1 blog-Geita


0 Comments