Header Ads Widget

HATIMAYE WALIOMFUNGIA MTOTO NASRA KWENYE BOKSI AKAFARIKI AKIPATIWA MATIBABU WAKABILIWA NA KESI YA MAUAJI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imewabadilishia mashtaka washitakiwa watatu katika kesi ya marehemu, Nasra Mvungi (4) waliokuwa wanakabiliwa na makosa ya kula njama na kufanya ukatili, sasa wanashitakiwa kwa kosa la kusababisha kifo cha mtoto huyo.

Watuhumiwa waliofikishwa, mahakamani hapo jana ni pamoja na baba mzazi wa Nasra, Rashid Mvungi (47), mkazi wa Lukobe na mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro pamoja na wanandoa Mariam Said (38) na mumewe Mtonga Omar (30), wakazi wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Kiwanja cha Ndege.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo, Mwendesha Mashitaka na Wakili wa Serikali, Sunday Hyera, kwa kushirikiana na wenzake, Wakili wa Serikali, Edgar Bantulaki na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Zabron Msusi, waliiomba Mahakama hiyo kuwasomea shitaka jipya la mauaji chini ya kifungu namba 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kwamba shitaka hilo halitawaruhusu washitakiwa kujibu lolote.


Alidai mahakamani hapo kuwa katika tarehe tofauti ya mwezi wa Desemba mwaka 2010 hadi mei 2014 katika maeneo ya Kiwanja cha Ndege washitakiwa hao kwa nia ovu walimtesa mtoto Nasra Mvungi na kumsababishia kifo chake Juni Mosi mwaka huu.

Hata hivyo, Hakimu Moyo alisema kwa mujibu wa sheria, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shitaka hilo na hivyo kuiahirisha hadi Juni 26, mwaka huu itakapofikishwa mahakamani hapo kwa kutajwa tena.

Watuhumiwa wote watatu walirudishwa rumande kwa kuwa shitaka hilo halina dhamana.

Post a Comment

0 Comments