Header Ads Widget

GHARAMA ZA MAISHA ZAPANDA GHAFLA SAMUNGE KWA BABU WA LOLIONDO


Gharama za maisha katika Kijiji cha Samunge wilayani Loliondo ambako maelfu ya watu wamekimbilia kuchimba dhahabu ambayo imegundulika, zimepanda kiwango cha kutisha hasa chakula na maji.


Katika machimbo hayo mapya maji yanapatikana mbali na eneo hilo, hivyo kufanya ndoo moja ya maji kuuzwa kati ya Sh500 na Sh2,000.

Maji katika eneo hilo lililotapakaa machimbo madogo yasiyo rasmi, yanasambazwa kwa kutumia punda ambao husafiri umbali mrefu na maji hayo pia hutumika kusafishia dhahabu kwa kuwa mto ambao madini hayo yanapatikana umeshakauka.

Kwa upande wa chakula, sahani ya wali inauzwa kati ya Sh3,000 na Sh6,000 huku mguu wa mbuzi ambao wanachinjwa hapo kwa wingi ni Sh8,000.

Mchungaji Mwasapila anena
Akizungumzia hali hiyo jana, Mchungaji Ambilikile Mwasapila aliiomba Serikali kuweka utaratibu wa wachimbaji hao kupata maji ili kazi yao isisimame.

Mwasapila aliyewahi kukaririwa akisema watu watajaa tena Samunge kuliko wale waliokwenda kwake kunywa kikombe cha dawa ya kutibu magonjwa sugu, alisema kupatikana kwa dhahabu katika eneo hilo ni sehemu tu ya ndoto yake.

Alisema mbali na dhahabu hiyo ya Samunge inayoanza kukusanya watu, bado kuna mambo makubwa yatakayotokea na maelfu ya watu kujaa zaidi.

“Hili la dhahabu sijawahi kulisema lakini kuna mengi yatatokea katika eneo hili la Samunge,” alisema.

Kama ilivyokuwa wakati wa tiba hiyo, katika machimbo haya bado hakuna mahala pa kulala, wachimbaji na watoa huduma katika eneo hilo wanalala kwenye mahema na kijijini Samunge.
Huduma za afya zinapatikana jirani na eneo la machimbo ambako safari hii kuna zahanati.
Vijana kwa wingi


Maelfu ya vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini wapo Samunge kuchimba dhahabu katika Mto uliokauka wa Karabaline huku wakisema wanapata dhahabu yenye ubora wa juu kuliko ya mahali pengine.

Baadhi ya wachimbaji kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Morogoro na Msumbiji, walisema dhahabu inayopatikana katika mto huo ambao umevamiwa kwa zaidi ya kilomita nne, inaelezwa imesambaa hadi katika mashamba na milima ya Kijiji cha Mgogo, Samunge.

Mchimbaji Mashaka Kasunga alisema dhahabu ya hapo haipatikani maeneo mengine nchini.
Alisema yeye na wenzake 30 wenyeji wa Ushirombo, Shinyanga ndiyo walikuwa wa kwanza kuchimba madini hayo Aprili mwaka huu baada ya kupata taarifa ya kuwapo kwake.

“Tulikuwa Singida machimboni ikaletwa dhahabu iliyotolewa mlimani hapa tukaiona ni bora sana ndipo tukaja tukachimba awamu ya kwanza na kupata gramu 116 na tukaenda kuuza,” alisema.
Mchimbaji John Kefa alisema hajui walipata gramu kiasi gani lakini wachimbaji wengine walipata kilo moja ya dhahabu ambayo waliuza zaidi ya Sh50 milioni.

Mchimbaji mzoefu, Sophita Malembeka alisema mashamba mengi yanayopakana na Mto na Mlima Mgongo yana dhahabu, hivyo kuomba waruhusiwe kuchimba pia kuupasua mlima.

Wachimbaji wengi walisema kwa siku zinapatikana gramu kati ya 100 na 200 za dhahabu ambazo katika eneo hilo zinauzwa hadi Sh60,000 kwa gramu.

Mchimbaji mwingine, David Selea alisema kwa wastani kama wakiwa na maji ya kutosha katika eneo la mita tano wamekuwa wakipata kati ya gramu tatu hadi tano kwa siku.

Mnunuzi wa madini, Charles Malongo kutoka Bariadi, Simiyu alisema kwa siku hununua hadi gramu 100 na dhahabu ya eneo hilo ni bora kwa asilimia 99.
CHANZO;MWANANCHI

Post a Comment

0 Comments