Wabunge wa bunge la Tanzania wamefurahishwa na utekelezwaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi EACOP
Wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameusifu mradi wa bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) kwa kutoa fidia nzuri kwa waliopitiwa na mradi huo na kutoa kipaumbele katika maeneo mengine ikiwemo utunzaji wa mazingira.Pia wabunge hao wameusifu mradi huo kwa kuwapa mafunzo waliopitiwa na mradi huo ya kilimo, ufugaji na elimu juu ya matumizi ya rasilimali fedha walizolipwa fidia.
Wakiongea wakati wa semina iliyoandaliwa na EACOP kwa ajili ya kutoa mrejesho wa hatua iliyofikiwa na mradi huo mpaka sasa kwa wabunge wa sekta ya Nishati na wengine waliohudhuria semina hiyo, mmoja wa wabunge hao Stephen Hasunga wa jimbo la Vwawa amesema tofauti na ‘propaganda’ zinazoenezwa, mradi huo upo tofauti sana na miradi mingine ambapo kwa kiasi kikubwa sana unazingatia sheria za nchi na zile za kimataifa katika utekelezaji wake.
“Tumeona kwa kiasi gani watu wamejengewa nyumba nzuri tofauti na zile walizokuwa wanamiliki hapo awali kabla ya kufikiwa na mradi,”
“Pia wamepewa chakula cha kukidhi mahitaji ya familia zao kwa kipindi cha mwaka mzima na mafunzo mbalimbali juu ya kilimo bora cha kisasa na ufugaji,”amesema Hasunga.
Naye mbunge Selemani Zedi wa jimbo la Bukene lililopo Nzega mkoani Tabora amesema yeye ni shuhuda wa yaliyofanywa na mradi huo kwa wananchi wake waliopitiwa na mradi huo.
“ Mradi umechukua zaidi ya ekari 400 za wananchi wangu, ambao wamepewa nyumba nzuri zilizobadilisha maisha yao ikiwa kama sehemu ya fidia,”
“Hao wanaosema mradi huu hauzingatii haki za binadamu waje waone na wanaosambaza propaganda hizi kwa sisi tulioguswa na mradi tunawashangaa kiukweli,”
Naye mbunge Esther Bulaya amesema serikali inatakiwa kuhakikisha kilichofanywa na mradi wa EACOP pia kinafanyika katika utekelezaji wa miradi mingine kwa kuwapa nafuu ya maisha wale wanaoguswa.
“Kuna vitu kama taifa tunaweza kujifunza katika ulipaji fidia kupitia mradi huu wa EACOP, ikiwemo juu ya ushirikishwaji wa wananchi wanaoguswa ambapo wanapaswa kuridhika na faida wanazopewa,”
“Miradi inapokuja isilete umaskini, bali watu wafurahie miradi hiyo,”
“Tumejifunza katika mradi wa EACOP, watu wamepewa nafasi ya kuchagua fidia ya nyumba au pesa na kunufaika na programu nyingine ikiwemo kupewa mbegu kwa ajili ya kilimo,”amesema.
Akizungumza kwa niaba ya serikali, Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato amesema serikali imeridhika na hatua zilizofikiwa mpaka sasa, ikiwemo suala la watu kulipwa fidia, utunzaji wa mazingira na maandalizi kiujumla ya mradi huo.
“Tunaendelea kusimamia kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa ili kuiletea nchi maendeleo kupitia mradi huu ikiwemo kunufaika na kodi mbalimbali zinazopatikana,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa EACOP Martin Tiffen, Martin Tiffen alisema kikao hicho cha ushirikishwaji kwa wabunge kilijumuisha awamu tatu zilizohusu maeneo muhimu ya mradi, ikiwa ni pamoja na watoa huduma wa ndani, ardhi, na masuala yanayohusu jamii na mazingira.
Amesema lengo la kukutana na wabunge wa kamati ya Nishati na wabunge wengine waliohudhuria mkutano huo katika ukumbi wa Pius Msekwa lilikuwa kuwapa mrejesho wa kilichofanyika na kinachoenda kufanyika.
Mwakilishi wa mradi huo kwa upande wa serikali kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC) Asiadi Mrutu amesema sehemu kubwa ya fidia imeshalipwa ambapo wananchi wanajiandaa kuondoka katika maeneo ya mradi kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi wa kuchimba mkuza ambao bomba hilo litapita.
Wakati wa kikao, Mkuu wa Kitengo cha Kujenga Uwezo kwa Watoa Huduma wa Ndani katika kampuni ya EACOP Martha Makoi, alitoa maelezo muhimu kuhusu watoa huduma wa ndani na kujenga uwezo, zaidi akisisitiza kuwapo kwa ushirikiano baina ya EACOP na Bunge.
Kwa mujibu wa afisa wa EACOP Fatuma Msumi , jumla ya watu 9898 wameguswa katika eneo litakalofukiwa bomba hilo, ambapo 9272 wameshalipwa fidia na sasa wanahitajika kuondoka katika maeneo hayo mwishoni wa mwezi wa 7.
Amesema mradi umekuwa ukiwashirikisha wananchi katika ngazi mbalimbali ambapo mikutano mingi imefanyika na wale waliokuwa na hoja zao za msingi walisikilizwa na hoja hizo kutatuliwa.
Kikao cha ushirikishwaji kwa Bunge la Tanzania kinaashiria hatua muhimu ya mradi wa EACOP, kuimarisha uwazi, ushirikiano, na majadiliano yenye kujenga na wadau muhimu wa mradi. EACOP itaendelea kuhakikisha inatimiza dhamira yake ya kufanikisha utekelezaji wa mradi huo, mwitiko chanya kutoka kwa Wabunge ni msaada wao unaongeza nguvu katika mradi.
0 Comments