JESHI la Kocha Mkuu wa Yanga Mtunisia, Nasreddine Nabi juzi liliingia kambini tayari kwa mchezo wa mwisho wa makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika huku likianza na program ya fiziki pekee.
Yanga katika mchezo huo, watacheza dhidi ya TP Mazembe Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa TP Mazembe, Lubumbashi nchini DR Congo saa 10:00 Jioni.
Katika mchezo huo, Yanga wataingia uwanjani kwa ajili ya kukamilisha ratiba pekee, kwani tayari wameshafuzu katika Kundi, D huku TP Mazembe wakitaka kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1.
Akizungumza na Championi Jumatano, Nabi alisema kuwa mchezo huo wanauchukulia umuhimu mkubwa, kwani wanazihitaji pointi za TP Mazembe ili wabakie kileleni katika msimamo ambao wana pointi 10 sawa na US Monastir waliofuzu hatua ya robo fainali.
Nabi alisema kuwa, kikosi chao kimeingia kambini juzi Jumatatu kikiwa chini ya kocha msaidizi Mrundi Cedric Kaze kwa kuanzana program ya fitinesi pekee kukimbia mbio fupi na ndefu kwa ajili ya kurejesha utimamu wa mwili wachezaji wao.
Aliongeza kuwa program hiyo iliwahusisha wachezaji waliobakia kambini wakiendelea na mazoezi huku wakiwasubiria wengine waliookuwepo katika majukumu ya timu za taifa.
“Nimewataka wachezaji wangu wote waingie kambini, ruhusa ikiwa kwa wachezai wale ambao wapo katika majukumu ya timu za taifa pekee na majeruhi.
“Lakini wote waliobakia wanatakiwa kuingia kambini, nashukuru katika hilo limefanikiwa hakuna mchezaji yeyote aliyekosekana kambini na wote wameripoti tayari kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya TP Mazembe.
“Wachezaji hao wameanza na program ya mazoezi ya fitinesi baada ya wachezaji kutoka katika mapumziko ambayo tulipawa mara baada ya mchezo dhidi ya US Monastir,” alisema Nabi.
MATOKEO YA YANGA CAF
Monastir 2-0 Yanga
Yanga 3-1 Mazembe
Bamako 1-1 Yanga
Yanga 2-0 Bamako
Yanga 2-0 Monastir
0 Comments