Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imemtaka yeyote anayeona kuwa kauli iliyotolewa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako imetishia maisha yake, afungue kesi.
Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua hatua polisi waliyoichukua kutokana na kauli aliyoitoa Mchungaji huyo kwamba waandishi waliomwandika vibaya watakufa kabla ya Machi mwakani.
“Kama kuna mtu anaona katishika na kauli hiyo aje afungue kesi milango iko wazi. Kama kuna mwandishi yeyote anayeona ametishika na kauli hiyo aje, kesi ikifunguliwa tutaifanyia kazi kwa sababu hadi sasa hakuna aliyelalamika,” alisema.
Kauli ya Mzee wa Upako aliitoa katika mahubiri yake ya Jumapili ikiwa ni mwendelezo wa majibu yake kutokana na tuhuma zilizoandikwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwamba alimfanyia fujo jirani yake.
Wakati huo huo, Sirro alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi wa madai ya kupotea kwa Bernard Saanane ambaye ni kiongozi wa Chadema. Kiongozi huyo anadaiwa kupotea tangu Novemba 18.
“Kuna watu wanasema wanataka ile miili ichunguzwe… lile ni tukio la Pwani na mwenye wasiwasi anaruhusiwa kuwasiliana na uongozi wa kule kwa sababu ule ni mkoa mwingine,” alisema.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum, Maxence Melo alisema atazungumzia suala hilo Ijumaa.
0 Comments