Header Ads Widget

Polisi Dar yawatia mbaroni watu 22 kwa kosa la uporaji katika magari



Kikosi maalumu cha kupambana na wizi wa kutumia silaha na wizi wa kutumia nguvu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kimewakamata watuhumiwa 22 kwa makosa ya kuwapora wenye magari na wapitanjia kwenye mataa ya kuongozea magari.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao, wamekuwa wakijiunda kwenye vikundi na kuwanyang’anya watu wenye magari na watembea kwa miguu mali zao kama simu za mikononi, kompyuta, saa na fedha.


Alisema ufuatiliaji ulifanyika na kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti, ambapo Desemba 11 mwaka huu huko Temeke maeneo ya Keko Magurumbasi na mataa ya Veta na Chang’ombe walikamatwa watuhumiwa 10 kwa makosa ya wizi kutoka maungoni na wizi kutoka kwenye magari.


Aliwataja baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Ayubu Amiri (19), mkazi wa Mtoni Mtongani, Shabani Fadhili(18) mkazi wa Keko, Herman Francis (26), mkazi wa Keko Magurumbasi na wenzao saba.


“Katika mahojiano watuhumiwa wamekiri kujihusisha na makosa mbalimbali yakiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha na kutumia nguvu,” alisema.


Aidha alisema uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa Herman Francis anakabiliwa na tuhuma za mauaji, ambapo Machi 20 mwaka huu alimchoma mtu kisu na kutoroka kusikojulikana. 


Wakati huo huo, Desemba 12 mwaka huu askari waliwakamata watuhumiwa wengine 12 kwa makosa ya wizi kutoka kwenye magari.


Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Sande Kassim (18), mkazi wa Keko, Emmanuel Abeli (21), Paulo Abeli(18), Jafari Nyerere (22), Hamis Salum (22), Hemed Idrisa(22) wote wakazi wa Keko na wenzao sita.

Post a Comment

0 Comments