Na Samira Said, DAR ES SALAAM
SIMBA SC imepitisha bajeti ya mwaka 2014/2015 ambayo ni Sh. Bilioni 3.008 katika Mkutano wake Mkuu leo, ambao pia umemfuta rasmi uanachama aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF), Michael Richard Wambura.
Mgombea huyo wa nafasi ya Urais katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Juni mwaka huu, Michael Wambura, pamoja na wanachama wengine 70 walifutwa rasmi uanachama wa klabu hiyo kutokana na hatua ya kufungua kesi kwenye mahakama za kawaida jambo ambalo ni kinyume na katiba.
Wanachama wa Simba SC wamemfuta uanachama Michael Wambura na kupitisha bajeti ya Mabilioni
Maamuzi ya kumfuta uanachama Wambura pamoja na wanachama wengine yalifikiwa kwa pamoja Leo katika Mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Wanachama 860 waliokutana jana hawakutaka agenda hiyo ya 12 ijadiliwe na badala yake wakisema kwa sauti kwamba wanachama hao wafutwe mara moja.
Agenda hiyo ya kuwajadili wanachama hao ambao awali walisimamishwa na Kamati ya Utendaji ilianza kujadiliwa saa 6:33 mchana na ilipofika saa 6:49 mchana Aveva alitangaza kwamba wanachama hao 71 wamefutwa uanachama wao kutokana na kwenda kinyume na ibara ya 55 ya katiba ya Simba.
Kabla ya kutoa maamuzi hayo, Aveva, alisema kuwa alipokea maoni mbalimbali kutoka kwa wanachama na aliamua kumtumia mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, Ramesh Patel, ili akutane na wanachama hao kwa ajili ya kupata suluhu.
Michael Wambura amefutwa uanachama Simba SC
Aveva alisema kuwa wanachama hao walielezwa na Patel kwamba wanatakiwa kwanza wafute kesi waliyoifungua Juni 23 mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam walikataa na hakuna kati yao ambaye alijitokeza kukanusha kuhusika na uvunjwaji huo wa katiba.
"Natangaza rasmi watu wote 71 sio wanachama wa Simba Sports Club kuanzia leo", alisema Aveva na kumaliza agenda hiyo iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na wanachama waliohudhuria mkutano huo.
Rais huyo alisema kwamba wanachama walikosea kwa kupinga bila kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa katiba ya Simba, TFF na Fifa.
Wambura ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa FAT sasa TFF hakuweza kupatikana katika simu zake za mkononi kuelezea maamuzi hayo yaliyochukuliwa na mkutano mkuu wa wanachama.
Pia mkutano huo mkuu wa wanachama wa Simba ulipitisha bajeti ya mwaka ujao wa klabu hiyo 2014/2015 ambayo itakuwa ni Sh. bilioni 3.008.
Akisoma bejeti hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Ally Suru, alisema kuwa Simba inatarajia kuingia Sh. bilioni 2.6 hivyo ina upungufu wa kiasi cha Sh. milioni 327.
CREDITS:BIN ZUBEIRY
0 Comments