Header Ads Widget

HII NI TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: RAIS AZUNGUMZIA JUU YA TUHUMA ZA KUMSAIDIA MWANAE BAADA YA KUKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA NJE YA NCHI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni mkusanyiko wa upuuzi mtupu madai kuwa yeye Rais alishiriki kumwokoa mtoto wake, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete
ambaye alikuwa amekamatwa na madawa ya kulevya nje ya nchi.


Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Urais ni taasisi kubwa sana nchini na hivyo yeye akiwa Rais hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo wanataka baadhi ya watu wanamsukuma ili ashiriki katika maneno hayo ya mitaani.


This is nonsense; ni mkusanyiko wa upuuzi. Sina muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna hiyo, amesema Rais Kikwete usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, wakati alipozungumza na Watanzania wanaoishi katika Marekani
kwenye Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington D.C.


Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa katika Marekani alitoa majibu hayo baada ya kuwa ameulizwa kuhusu madai yaliyotolewa Julai Mosi, mwaka juzi, 2012 na Katibu Mkuu wa Chama cha CHADEMA, Wilbroad Slaa, madai hayo yamempeleka mahakamani.


Amesema Rais Kikwete: “Hatuwezi sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa kushiriki upuuzi na ujinga. Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na watu ambao kazi yao usiku na mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda yetu ambayo imefanikiwa sana katika kubadilisha hali ya maisha ya Watanzania.”


Amesisitiza Rais Kikwete: “Urais ni taasisi kubwa sana. Rais wa nchi yetu hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mitaani. Kwanza huyo Ridhiwani amemfikisha Slaa kortini na mpaka leo hata kesi yenyewe haijatajwa.”


Kuhusu swali jingine aliloulizwa kuhusu suala hilo, kuwa Rais Kikwete alitia saini mikataba 12 na uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa Ridhiwani, Rais Kikwete amesema: “Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi kufikiria hata kuiweka rehani.


Haya ni maneno ya kipuuzi tu, yenye kutafuta kututoa kwenye ajenda zetu nzuri. Hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu kwenye mambo ya maana ya kuleta mabadikio katika ustawi wa Watanzania.”





Imetolewa na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu Dar es Salaam.
04, Agosti, 2014

Post a Comment

0 Comments