Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wassira, ameibuka na kupinga kauli ya Jaji Joseph Warioba kuhusu umri wa mgombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Warioba alikaririwa juzi akisema taifa la Tanzania linastahili kuongozwa na vijana wenye nguvu ya mwili na akili.
Wassira, Mbunge wa jimbo la Bunda, ambaye jina lake linatajwa kuwa mmoja wa wanaowania nafasi ya urais uchaguzi mkuu wa 2015, alisema kuwa kauli ya Warioba inaweza kuwa ni maoni yake binafsi, lakini hakuna sifa za uzee wala kijana katika kuwania nafasi kubwa ya nchi kwa kutumia vigezo hivyo.
Akiongea kwa njia ya simu, Wassira ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), alisema;
“Uzee siyo sifa ya kuwa rais mzuri au ukiwa kijana pia siyo sifa ya kuwa rais mzuri, kwani kura zinapigwa na Watanzania, wapo wazee na vijana wote wanapiga kura, kinachotakiwa kuangalia hapa, je, huyu anayetaka urais ni mzalendo wa kweli, anaijua vema nchi yake ni muadilifu na anajua matatizo yanayowakabili vema Watanzania wa mjini na vijijini, siyo kukimbilia kusema kundi fulani lipewe nafasi.”
Alisema anaweza kupatikana kijana mzuri ambaye anaweza kuivusha nchi kutoka hapo ilipo hadi panapotakiwa lakini kubwa hapa ni kuangalia uwezo wake kijana huyo badala ya kuona ukijana kuwa moja ya sifa za urais.
“Kuna wazee wenye busara, wanaijua vema nchi hii, waadilifu, wanayajua vema matatizo ya Watanzania, anaijua vema nchi yake pasipo kutembezwa, na ni wazalendo wakubwa, je, utaachaje kumpa nafasi mtu kama huyu eti kwa vile ni mzee,” alihoji Wassira.
Warioba alikaririwa akisema umefika wakati wa wazee kung’atuka na kuwaachia vijana huku akisema sifa ya rais ajaye anapaswa kuwa kijana, kauli ambayo inapingwa na Wassira.
Wassira alisema kuwa miongoni mwa matatizo yanayowakabili Watanzania ambayo yanapaswa kutazamwa na rais ajaye, kubwa ni kutambua kuwa theluthi moja ya Watanzania wanaishi katika umasikini mkubwa uliokithiri na kuwekeza katika elimu hasa ya sayansi ambayo itasaidia kujibu baadhi ya matatizo.
“Huwezi kusema unataka urais wakati haujui matatizo ya Watanzania, ukifikiria kuwa rais wa nchi kwa sasa lazima uhakikishe rasilimali za nchi zinatumika kusaidia sekta inayoajiri watu wengi hasa kilimo, uvuvi pamoja na ujenzi wa viwanda ili uweze kujibu tatizo la ajira,” alisema na kuongeza.
“Kuna wasomi wengi ambao wanazalishwa kila mwaka nchini, hatuwezi kusema wote wataajiriwa viwandani bali lazima tutengeneze mazingira ya kuwawezesha kujiajiri wenyewe hasa kwa kuelekeza rasilimali za nchi katika sekta muhimu kikiwamo kilimo, ufugaji na ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao ya wakulima,”alisema Wassira.
Mbali na Wassira, wengine wanaotajwa kuwania urais ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa, aliyewahi kuwa waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye juzi alikaririwa akitangaza kuwa kwa asilimia 90 amefikisha vigezo vya kuwa mgombea urais kupitia CCM.
Waziri Wassira yuko jimboni Bunda kwa ziara ya kibunge ambapo pamoja na mambo mengine amewaambia wapiga kura wake mpango wa serikali ambao umepitishwa hivi karibuni na mchakato wa katiba mpya unavyoendelea.
Na George Marato
0 Comments