
Baadhi ya wanafunzi wa DIT waliandamana mpaka Ofisini kwa Waziri wa Sayansi na Teknolojia kupeleka kilio chao.
Wanafunzi wa Taasisi ya Uhandisi Dar Es Salaam (Dar Es Salaam Institute of Teknology (DIT) wapatao 3,402 wapo katika mgomo wa siku mbili wakiomba uongozi wa chuo, kuwaruhusu wanafunzi wapatao 684 kufanya mitihani ya kumaliza muhula wa masomo.
Rais wa wanafunzi wa chuo hicho Himida Elihuruma alisema kuwa, mgomo huo baridi umesababishwa na kukosekana kwa usajili wa wanafunzi hao kwa kuwa wanadaiwa pesa ya ada, na hivyo wanafunzi wote wameazimia kugoma kufanya mitihani ili wale ambao hawajasajiliwa kufanya mtihani basi waruhusiwe kufanya mitihani.
Wanafunzi hao waliomba wenzao waruhusiwe wafanye mtihani na matokeo yao ndio yazuiliwe kwa sababu hawajamaliza ada, na hivyo wameamua kwenda kwa Waziri wa Sayansi Teknologia kwa Profesa Makame Mbarawa kwa kumueleza kilio chao.

Polisi wa kutuliza ghasia (FFU) wakiwa wametinga katika Wizara ya Sayansi na Teknologia kuwazuia wanafunzi kulisogelea jengo hilo.
Naye Afisa Uhusiano wa chuo hapo Amani Kakana alisema kuwa, sio wanafunzi 684 ndio walizuiliwa bali ni wanafunzi 180 ndio wamesimamishwa, kwa mujibu wa sheria za mitihani wamezuiliwa mpaka watakapomaliza ada, na wakimaliza kulipa ada basi watafanya mitihani mwezi Julai mwaka huu.
“Nawashangaa wanafunzi hao kukimbilia kwa waziri wakati hapa shuleni kuna bodi ya chuo, Rais wa wanafunzi ni mjumbe katika bodi hiyo, sasa wanapokurupuka kwenda kwa waziri ni ngazi ya juu sana ambayo wao kwa sasa hawapaswi kwenda huko,” alisema Kakana.
0 Comments