Header Ads Widget

MSAFARA WA MWENGE WAPATA AJALI MBEYA, ASKARI MMOJA AJERUHIWA,BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI



MSAFARA wa Mwenge wa Uhuru ambao upo mkoani Mbeya, umepata ajali katika Wilaya ya Rungwe iliyosababishwa na mwendo kasi ambao ulipelekea gari ya Jeshi la Polisi mkoani humo yenye namba PT 1631 kugongwa na kumjeruhi Askari mmoja ambaye ametajwa kuumia vibaya FikraPevu imejulishwa.


Aidha, taarifa za awali kutoka vyanzo vyetu vya habari vimedai kuwa, ajali hiyo ilitokea wakati msafara huo ukiwa unaelekea katika kuzindua mradi wa shule ya daraja la Mungu, ambapo gari moja ambayo haikutambulika namba zake iligonga gari ya polisi na kusababisha Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kujeruhiwa vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili wake.


Hata hivyo, baadhi ya waandishi wa habari walioteuliwa kuambatana na msafara huo, wamedai kuzuiwa kuripoti tukio hilo na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ambapo tukio hilo lilitokea Mei 31, 2014 saa saba mchana katika Wilaya ya Rungwe mkoani humo.


Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ahmed Msangi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema “Ajali sio kubwa sana…ni ndogo na wakati huu magari yanakuwa kwenye msafara kwa ajili ya zoezi hilo na kule kuna vumbi kweli, kwahiyo gari la polisi lilisimama kwa pembeni likiwa na Askari wengine (FFU) ambao mmoja alijeruhiwa na gari moja lililokuwa kwenye msafara."


Alisema ajali hiyo imesababishwa na vumbi lililopo katika barabara hiyo na sio mwendo kasi na kutaja gari ya polisi iliyopata ajali kuwa ni PT 1631 ambayo ilipinda kidogo kutokana na ajali hiyo na sasa mwenge unaendelea na ziara yake mkoani hapa.


“Huyo dereva alitaka kuikwepesha ile gari lakini katika harakati hizo aliigonga ‘kidogo’ gari ya polisi na kumgonga Polisi mwenye namba, J 2649 PC Grace, baada ya hapo alianguka na tukampeleka hospitali na sasa hivi anaendelea vizuri hajavunjika isipokuwa tuliona ni vyema tukampeleka katika Hospitali ya Rungwe ili apatiwe matibabu kidogo” alisema Msangi.


Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispin Meela, alikana kutokea kwa tukio hilo, licha ya kutokea katika wilaya yake.


Chanzo: fikrapevu

Post a Comment

0 Comments