Header Ads Widget

HATIMAYE MABOMU YARINDIMA KUTAWANYA WAFANYABIASHARA WAKATI WA BOMOABOMOA KITUO CHA MWENGE


Jeshi la Polisi limelazimika kuwatawanya wafanyabiashara wadogo katika Kituo cha daladala cha Mwenge jijini Dar es Salaam, baada ya kutokea kwa vurugu ya kupigana na kurushiana mawe baina ya kikundi cha watu waliofika katika kituo hicho kilichojulikana kwa jina la Matembo na kuanza kuwadai fedha ya ushuru bila kufuata utaratibu.

FikraPevu imeshuhudia wafanyabiashara hao wakirushiana mawe kwa muda na kundi hilo, kabla ya Polisi kufika na kuanza kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi na huku wengine wakiwa na silaha za moto.


Wakiongea na FikraPevu leo Jumanne Juni 3, 2014 wafanyabiashara hao wamedai kuwa kikundi hicho kimekuwa kikiwadai fedha kati ya shilingi elfu tatu hadi elfu nane kuanzia jana mchana katika kituo hicho bila kuwapatia risiti kinyume na agizo na Manispaa ya Kinondoni lilivyowapangia.


Baadhi ya wafanyabiashara hao, Hamisi Abdala, na Amani Mbaga, wamesema tangu kundi hilo lilipofika kituoni hapo na kuanza kuwadai fedha waliwaeleza kuwa hawana, ndipo walipoanza kutofautiana kauli na kugundua kuwa ni matapeli kwani waliambiwa na kundi hilo kuwa eneo hilo lipo kwa ajili ya wafanyabiashara.

“Tupo tayari tufanye kazi na kuwalipa Manispaa lakini sio hawa wababaishaji kwani kazi ni ngumu wanatudai elfu tatu na hawatupi risiti, kwa kweli sisi tumechoshwa na hali hii, hili ndilo eneo tunalojipatia kipato na wakisema watuondoe hapa maisha ya Dar es Salaam ni magumu, chumba ni elfu hamsini na hizi fedha tunazozipata ndizo zinazotusaidia tukiwa na familia zetu” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.
FikraPevu imewasiliana na aliyekuwa kiongozi wa kutoza ushuru katika kituo hicho, Juma Kesi, ambaye amekataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yupo Kilosa mkoani Morogoro na hana taarifa zozote juu ya vurugu hizo.
Malalamiko ya wananchi
Wakazi wa jiji hilo wanaotumia kituo hichowamejikuta katika adha kubwa ya usafiri baada ya kituo hicho kuzuiwa kutumika na kuhamishiwa Makumbusho.


Akizungumza na FikraPevu, Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera, amesema stendi hiyo imehamishwa kupisha upanuzi wa barabara na kuongeza kuwa magari yote yenye kutumia kituo cha Mwenge yanatakiwa kutumia kituo cha Makumbusho.


Baadhi ya abiria pamoja na madereva wamesema utaratibu huo umefanywa ghafla hivyo kuleta adha kubwa na usumbufu wa usafiri ikiwa ni pamoja na kuogezeka kwa gharama za kusafiri.


Vibanda na maduka vyabomolewa
Magreda ya Manispaa ya Kinondoni yamefanya shughuli za kubomoa vibanda, maduka, stendi za kupumnzikia abiria, vyoo vya kulipia na baadhi ya Ofisi za watu binafsi, kwa ajili ya kupisha upanuzi wa barabara hiyo.


Mapema wiki iliyopita, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) iliridhia kuhamisha kituo hicho kwenda katika eneo la Makumbusho kwa ajili ya kupisha upanuzi wa eneo hilo ambao umeelezwa kuwa mdogo.


CHANZO;FIKRA PEVU

Post a Comment

0 Comments