Kikosi cha Simba.
BAADA ya Simba kung’ang’aniwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amesema kuwa baada ya sare hiyo nguvu na hamu yao ni kushinda dhidi ya Azam FC.
Jumapili Simba itakuwa na mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports Cup (ASFC) dhidi ya Azam FC, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mgunda alisema, kweli wamefeli malengo yao ya kupata pointi tatu dhidi ya Namungo FC, ila sasa nguvu na akili zao wanazielekeza kupata ushindi dhidi ya Azam FC.
“Tumepata sare jambo ambalo siyo baya japo hatukipanga hivyo lengo lilikuwa pointi tatu, kwa sasa tuseme tu pamoja na matokeo haya kuna mengi ya kujisifu ila kuna mengi pia ya kufanyia kazi kwenye mazoezi.
“Tunajua mchezo uliopo mbele yetu ni muhimu sana kwani tunahitaji kupata ushindi na kusonga mbele, hivyo tuna kila sababu ya kuhakikisha tunafanyia kazi mapungufu ya leo ili tutimize lengo letu la kupata ushindi dhidi ya Azam,” alisema Mgunda.
Kwa upande wao Azam kupitia kwa Kocha Msaidizi, Kally Ongala ameweka wazi kuwa, hawapo tayari tena kuona wakifungwa na Simba kwenye mchezo ujao, kwani wanahitaji sana kuchukua kombe hilo.
Ongala alisema: “Tunaijua Simba ni timu nzuri sana ila sisi tupo imara na timu yetu kuwafunga Simba tumeshajiandaa kila namna ya kucheza nao ili tuweze kuwafunga na kusonga hatua ya fainali.“Simba imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa ila kiukweli tunawapongeza kwa hatua walioishia. Kuhusu kucheza na sisi tunafahamu bado wana morali kubwa hivyo watataka kucheza kwa nguvu sana ila tutakabiriana nao ili tuweze kutinga fainali.
“Tunajua namna ya kucheza nao kwenye ligi na kwenye hii FA, tutaenda kushindana nao ili nasi tuwaonyeshe kama tunaweza.”
Stori na Musa Mateja
0 Comments