Header Ads Widget

Bondia Karim Mandonga Apima Uzito, Kupanda Ulingoni Leo Dhidi Ya Lukyamuzi

Bondia Karim Mandonga (kulia) baada ya kupima uzito na mpinzani wake Kenneth Lukyamuzi

BONDIA Karim Mandonga jana alifanikiwa kupima uzito tayari kwa pambano lake dhidi ya Kenneth Lukyamuzi, ambalo linatarajia kupigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Kasarani hapa Nairobi, Kenya.

Mandonga na Lukyamuzi walipima uzito Machi 24, 2023 kwenye ofisi za makao makuu ya DStv ambao wanatarajia kurusha pambano hilo lisilokuwa la ubingwa ambalo litapigwa kwa raundi nane kwenye uzani wa Super Middle.

Mandonga ambaye amekuwa maarufu jijini hapa kufuatia kumtwanga kwa TKO ya raundi ya tano, Mkenya, Daniel Wanyonyi katika pambano ambalo lilipigwa Januari, mwaka huu katika Ukumbi wa AICC Nairobi.


Mara baada ya kupima uzito, Mandonga kama ilivyokuwa kawaida yake ya kuchimba mikwara alimwambia mpinzani wake atahakikisha anampiga katika hali yoyote huku akisisitiza ngumi yake ya Mlunga Mbunga itafanya kazi yake kwa uhakika mkubwa.

“Huyu hawezi kusumbua kwa sababu saizi yake ni Wanyonyi ila kaja nitampandisha na yeye aonekane lakini hataki anapigwa akitaka anapigwa, niwaambie mashabiki wangu wa hapa Kenya na Watanzania waliopo hapa wajitokeze kwa wingi katika pambano hilo,” alisema Mandonga.


Kwa upande wa mpinzani wake alisema kuwa hataki kuongea sana zaidi ya kuacha mikono yake ifanye kazi kesho (Jumamosi) atapata matokeo mazuri kwenye pambano hilo.

Baraka Sherukindo ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Masoko wa DStv Afrika Mashariki alisema anaamini pambano hilo litaamsha hali mpya kwa wateja wao kutokana na kukua kwa mchezo huo.

Wengine waliopima uzito ni George Bonabucha atakapanda ulingoni na Michael Daries, Zawadi Kutaka na Praxides Oduori wa Kenya, Fatma Yazidu na Consalata Musanga wakati Nick Otione akitarajia kucheza na Hassan Ndonga wa Tanzania.

Post a Comment

0 Comments