Mkuu wa wilaya ya Bariadi Erato Sima ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo.
JESHI la polisi mkoani Simiyu limefanikiwa kuwakamata watu saba wanaodhaniwa kuwa wauwaji wa aliyekuwa mlemavu wa ngozi (albino) Munghu Mugata (40) aliyeuwawa kwa kukatwa mapanga mnamo mwezi mei huko katika kijiji cha Gasuma kata mwaubingi wilayani bariadi.Akiongea na waandishi wa habari ofisi kwake, mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa ambaye pia ni mkuu wa mkoa Paschal Mabiti, alisema kuwa kati ya watuhumiwa hao mmoja ni mganga wa jadi.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kudawa Yelema (52) ambaye ni mganga wa jadi, Sitta Maduhu (39), Jasamila Sungwa (42), Mpamba Saguda (18), Dede Madono (54), Majeshi Sunja (38), pamoja na Mabula Bindondo (52) wote wakulima na wakazi wa kijiji cha Gasuma
Alisema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na wasamalia wema, liliendesha msako mkubwa wa kuwasaka wahusika wa tukio hilo, ambapo lilifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa hao saba.
Alibainisha kuwa Dede Madono (54) mmoja kati ya watuhumiwa hao, aliugua ugonjwa wa maralia wakati akiwa maabusu na kupelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Bariadi, ambapo alifariki dunia akiwa hospitalini hapo akipatiwa matibabu.
Mabiti alieleza jeshi la polisi bado linaendelea kumsaka mdhamini wa mauaji hayo, pamoja na kutafuta sehemu viungo vya mlemavu huyo wapi vilipelekwa ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani na kujibu tuhuma zinazowakabili.
Aidha mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa marehemu Lughata alimwacha mtoto wake Tiri Kulwa (8) darasa la kwanza, ambaye alieleza kuwa kwa sasa mtoto huyo anahudumiwa na halmashauri ya Wilaya ikiwemo kumsomesha.
Hata hivyo mkuu huyo alizitaka wilaya zote kuhakikisha wanakusanya takwimu sahihi za watu wenye ulemavu wa ngozi ikiwa pamoja na kutambua mahali wanapoishi.
Alisema mbali na kuagiza kukusanya kwa takwimu hizo viongozi ngazi ya vijiji na kata wameagizwa kuhakiksha albino wote wanawekewa ulinzi wa kutosha kwa kushirikina na wanachi katika maeneo wanakoishi.
Sambamba na hilo mabiti alitoa onyo kali kwa watu wanatenda matukio hayo na kuwataka kuacha mara moja, huku akieleza kwa atakayebainika kutenda unyama huo utakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Tukio hilo lililotokea mei 12 mwaka huu katika kijiji ca Gasuma kata ya mwaubingi Wilaya ya Bariadi Mkoani hapa, baada ya mlemavu wa ngozi Mugata kuvamiwa na watu wasiojulikana majira ya saa 8 usiku akiwa amelala nyumbani
0 Comments