Header Ads Widget

WASIWASI UMEIGHARIMU TAIFA STARS- NOOIJ



Na Boniface Wambura, Maputo
Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema moja ya sababu za kikosi chake kupoteza mechi dhidi ya Msumbiji (Mambas) ni wachezaji wake kucheza kwa wasiwasi katika kipindi cha kwanza.
Taifa Stars iliruhusu bao la kwanza sekunde chache kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kutafuta tiketi ya kucheza hatua ya makundi iliyochezwa leo (Agosti 3 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto hapa Maputo.
Bao hilo katika mechi hiyo iliyomalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3 lilifungwa kwa kichwa na mshambuliaji Josemar Machaisse.


Nooij alisema wasiwasi katika kipindi cha kwanza ndio ulioipa Msumbiji fursa ya kutawala mechi hiyo katika kipindi hicho na kukimalizia ikiwa mbele kwa bao hilo la mshambuliaji huyo wa klabu ya Bravos de Maquis ya Angola.


Alisema timu yake ilitulia kipindi cha pili baada ya kumuingiza Amri Kiemba badala ya Khamis Mcha. Pia alilalamikia bao ambalo Taifa Stars ilifunga dakika ya 16 kupitia kwa John Bocco lakini likakataliwa na mwamuzi Dennis Bate kutoka Uganda.


Aliongeza kuwa mchezaji Elias Pelembe aliyeifungia Msumbiji bao la pili dakika ya 83 kwa mpira wa adhabu nje ya eneo la hatari ndiye aliyemaliza mchezo huo. Pia ni mchezaji huyo aliyebadili matokeo ya mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam ambapo Msumbiji ilisawazisha dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho.


Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, na ambayo ilicheza vizuri kipindi cha pili ilipata bao lake dakika ya 78 na Mbwana Samata kwa shuti la pembeni akiwa nje ya eneo la hatari na kumshinda kipa Ricardo Campos.
Matokeo hayo yameipeleka Msumbiji katika kundi C lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia. Mechi za hatua ya makundi kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco zitaanza kuchezwa mwezi ujao.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Timu itakayosonga mbele itaingia kwenye kundi lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia.
Taifa Stars inarejea Dar es Salaam leo (Agosti 4 mwaka huu) saa 8 mchana kwa ndege ya Air Tanzania.
Kikosi cha Stars kilipangwa hivi; Deogratias Munishi, Said Moradi, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Erasto Nyoni, Mwinyi Kazimoto, Mcha Khamis/Amri Kiemba, John Bocco/Simon Msuva, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu/Mrisho Ngasa.

Post a Comment

0 Comments