KLABU ya Barcelona imepata ahueni kwa kurejea mazoezini kwa nyota wa kimataifa wa Brazil, Neymar baada ya kupona majeruhi ya mgongo yaliyokuwa yakimsumbua. Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alikwamia katika hatua ya robo fainali katika michuano ya Kombe la Dunia kufuatia kugongana na beki wa kimataifa wa Colombia Camilo Zuniga katika mchezo uliozikutanisha timu hizo. Lakini baada ya kupita wiki sita, Neymar sasa amejiunga na kikosi kizima cha Barcelona kwa ajili ya mazoezi leo akiwa sambamba na nyota mpya Jeremy Mathieu na Xavi ambao nao walikuwa majeruhi. Hata hivyo beki mpya aliyesajiliwa Thomas Vermaelen ambaye ametokea Arsenal kwa kitita cha paundi milioni 15 ameshindwa kufanya mazoezi na wenzake leo na badala yake alifanyiwa vipimo zaidi kuangalia majeruhi yanayomsumbua ambayo aliyapata katika Kombe la Dunia. Barcelona inaanza kampeni zao za La Liga Agosti 24 dhidi ya Elche na huo utakuwa mchezo wa kwanza kwa kocha Luis Enrique.
0 Comments