Header Ads Widget

UNAAMBIWA JWTZ KUANIKA TENA ZANA ZAKE ZA KIVITA JIJINI DAR KATIKA KONGAMANO KUBWA LA KIJESHI



JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linatarajiwa kufanya maonesho ya zana zake za kivita zinazotumiwa na askari wa nchi kavu kuanzia Julai 14 hadi 16, mwaka huu wakati wa kongamano kubwa la kijeshi ambapo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo nchini.

Kampuni zaidi ya 30 zinazotengeneza silaha na vifaa vya kijeshi kutoka ndani na nje ya nchi zitaonyesha bidhaa zao katika Kongamano hilo.

Akizungumzia kongamano hilo litakalofanyika kwenye Ukumbi wa wa Milimani City, Dar es Salaam, Julai 14 hadi 16, mwaka huu, mkuu wa kamandi ya Jeshi la Nchikavu, Meja Jenerali Salim Kijuu alisema jana kuwa viongozi mbalimbali wakiwemo wadau wa jeshi watashiriki.

“Kampuni 32 za kimataifa zinazozalisha na kuuza silaha na vifaa vya kijeshi zimethibitisha kushiriki katika maonyesho hayo. Viwanda vyetu vya kijeshi na vile vya kiraia vinavyozalisha silaha za kijeshi pia vitashiriki,” alisema Kijuu.

Alibainisha kuwa Tanzania itatumia fursa hiyo kulitangaza jeshi lake katika jumuiya za kimataifa, hasa katika kipindi ambacho linaelekea kwenye maadhimisho ya miaka 50 tangu lilipoanzishwa.

Alisema majeshi yatakutana kujadili jinsi ya kukabiliana na changamoto za sasa za ulinzi na usalama hasa eneo la Afrika Mashariki ambalo linakabiliwa na changamoto ya uvuvi haramu, uharamia na jinsi ya kulinda maliasili za Taifa.

Brigedia Jenerali Simon Mumwi alisema ingawa maonyesho hayo yanahusu silaha na zana za kijeshi, hayana lengo la kuzitisha nchi jirani, bali kuimarisha uhusiano.

“Tunawaalika wenzetu ili waje tupeane ujuzi na uzoefu wa changamoto za kiusalama na siyo kuwaonyesha kwamba na sisi tupo,” alisema Mumwi.

Kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya JWTZ Agosti, mwaka huu, kutafayika mazoezi makubwa ya kijeshi Arusha.
CREDIT: Eddy blog

Post a Comment

0 Comments