Watu wawili wanaoshukiwa kuwa majambazi wameuawa eneo la Temeke Wailesi, jijini Dar es Salaam wakati wakipambana na polisi kwa kurushiana risasi.
Katika tukio hilo pia askari aliyekuwa akipambana na majambazi hao aliuawa.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 5 asubuhi jana, wakati majambazi hao waliokuwa wanne wakiwa kwenye usafiri wa pikipiki mbili maarufu kama bodaboda, kuvamia nyumba ya mkazi wa eneo hilo, Ali Hassan na kupora kiasi cha Shilingi milioni mbili na vitu vingine vya thamani.
Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, aliiambia NIPASHE kuwa askari wa kikosi maalum cha kupambana na ujambazi, walikuwa kwenye doria na baada ya kupata taarifa ya tukio hilo hilo, walikwenda moja kwa moja kwenye nyumba hiyo.
Alisema wakiwa njiani wakikaribia eneo la tukio, walikutana na majambazi hao waliokuwa wanakimbia na wakati wakipambana nao, walianza kurusha risasi hovyo na kumpiga askari wa upepelezi, Koplo Busagara, ambaye alifariki hapo hapo.
Kufuatia tukio hilo, askari hao walijibu mapigo kwa kuwarushia risasi na majambazi hao ambapo walifanikiwa kuwaua majambazi wawili waliofariki papo hapo.
Aliwataja majambazi waliofariki kuwa ni Juma Shabani, mkazi wa Mbagala Mtoni na Ali Mohamed, mkazi wa Mbagala.
Alisema katika tukio hilo, majambazi wengine wawili walikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka kwa kuanzisha msako wa nyumba kwa nyumba ili kuwanasa wahalifu hao.
Alitoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa ya watu wanaohisi kuwa wanajihusisha na mambo ya kihalifu.
Aliongeza kuwa askari aliyeuawa amekufa kishujaa akiwa anapambana kupigania mali za wananchi na kwamba katika mazishi yake atapewa heshima zote za kijeshi.
Kamishna Kova alisema miili ya watu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Wakati huo huo, askari wa Jiji, Stefano Komba (35), amefriki duniani baada ya kushambuliwa na wafanyabishara wadogo maarufu kama wamachinga wakati akiwa katika operesheni safisha jiji eneo la Kariakoo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo watu 22 wamekatwa.
Hata hivyo, waliachiwa baada ya upelelezi ambapo wawili kati yao wamebadilishiwa mashitaka yao na kushitakiwa kwa kosa la mauaji badala ya shambulio.
0 Comments