KOCHA Mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema anataka kuona timu yake ikipata ushindi wa mabao mengi zaidi, huku akipanga kutengeneza muunganiko wa safu ya ushambuliaji na kiungo.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa kumalizika kwa Simba kuwafunga Power Dynamos ya nchini Zambia mabao 2-0 yaliyofungwa na Willy Onana na Fabrice Ngoma.
Mchezo huo ulipigwa juzi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika Tamasha la Simba Day.
Onana anayecheza nafasi ya ushambuliaji na Ngoma kiungo, ni miongoni mwa nyota wapya kikosini hapo.
Akizungumza na Spoti Xtra, Robertinho alisema haikuwa rahisi kwa wachezaji wake kupata matokeo ya ushindi katika mchezo huo, hivyo anawapongeza kwa kushika maelekezo na mbinu zake mazoezini.
Robertinho alisema kilichobakia hivi sasa kwa wachezaji wake ni kuwatengenezea muunganiko mzuri kwa kuanzia safu ya kiungo kwenda kwa washambuliaji ili watengenezeane nafasi nyingi za kufunga mabao.
Aliongeza kuwa safu ya kiungo na ushambuliaji inahitaji kuongezewa mbinu zitakazowafanya wacheze kwa kuelewana, akiamini kama wakielewana basi ipo siku atapata ushindi wa mabao zaidi ya matano katika mechi moja.
“Kama unavyofahamu wachezaji walikuja kwa makundi kambini tulipokuwepo Uturuki tukijiandaa na maandalizi ya msimu ujao, hiyo ni baada ya usajili wa baadhi yao kuchelewa.
“Ninaendelea kuiboresha kombinesheni hiyo ya viungo na washambuliaji ili icheze vizuri, licha ya kuonesha mabadiliko ya haraka katika mchezo dhidi ya Power Dynamos.
“Vitu vichache tu ndio wanavyotakiwa kuongezewa viungo na washambuliaji hao ikiwemo kutengenezeana nafasi za kufunga, na kabla ya ligi kuanza vijana wangu watakuwa wapo vizuri,” alisema Robertinho.
0 Comments