Mshambuliaji Kylian Mbappe.
KLABU ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa imekubali dau la Al Hilal ya Saudi Arabia la Euro Milioni 300 (Sh bil 811.5) kwa ajili ya kumnunua mshambuliaji Kylian Mbappe.
PSG wametoa ruksa kwa Al Hilal kuanza mazungumzo na Mbappe baada ya kukubali ofa hiyo. Hata hivyo inadaiwa Mbappe atachomoa kwani nia yake ni kuendelea kukiwasha Ulaya.
PSG wanaamini kwamba Mbappe ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja tayari ana makubaliano na Real Madrid ili kujiunga nao msimu ujao ndio maana anadengua kusaini mkataba wa nyongeza hivyo ameambiwa achague kusaini au kuondoka huku akiondolewa kwenye kikosi kilichosafiri kwenda Pre-season.
Juzi matajiri wa Uarabuni, waliamua kuweka mezani mkwanja huo mrefu ili kumnunua Mbappe baada ya kushindwa kumpata Lionel Messi lakini inaonekana ngumu kwa Mbappe kukubali.
Wakati huohuo, Mbappe amevunja ukimya wake kuhusu ofa ya Al Hilal ya uhamisho wa rekodi ya dunia na kutuma ujumbe kwa mchezaji maarufu wa kikapu Giannis Antetokounmpo.
Nyota huyo wa Milwaukee Bucks alichapisha picha yake kwenye Twitter akiandika “Al Hilal unaweza kunichukua. Ninafanana na Kylian Mbappe” (akaweka na emoj mbili za kucheka).
Muda mfupi baada ya chapisho hilo kuonekana moja kwa moja, Mbappe alijibu kwa kutuma emoj 13 akicheka hadi machozi.
0 Comments