Kwa mara nyingine tunamshukuru Mungu, tunaivuta pumzi ya bure kutoka kwake. Ametupa uzima tunakutana tena Julai 17, 2023 kupeana darasa la uhusiano na maisha ya kila siku.
Wiki iliyopita tulijifunza juu ya umuhimu wa kuridhika na uliyenaye. Maana ukimtenda uliyenaye kwa tamaa za muda mfupi, unaweza na wewe kuja kutendwa huko uendako. Nilisema malipo ni hapahapa duniani!
Leo tunakwenda kuitazama mada iliyopo mezani. Ndugu zangu, kama ingekuwa ni mtihani basi tunaweza kusema hakuna mtihani mgumu kufaulu kama wa kumpata mwenza sahihi wa maisha. Wengi sana wamefeli, najua wewe pia ni shahidi katika hili.
Kwa kudhamiria au kutodhamiria, wengi hujikuta wameingia kwenye ndoa na mtu ambaye si sahihi. Ukifanya utafiti kwa sasa, watu waliofunga ndoa miaka kumi au zaidi iliyopita, utagundua kati ya wanandoa kumi, wanne au watano pekee ndiyo watakuwa wanafuraha na amani katika ndoa zao.
Wawe na muda mfupi au mrefu tangu waingie kwenye ndoa, wanachokishuhudia kwa sasa ni tofauti na matarajio waliyokuwa nayo. Hii inatokana na nini? Wapendanao wengi wanapokuwa kwenye uchumba, huwa hawatumii vizuri nafasi hiyo kufanya ‘rehearsal’.
Kwa kawaida, kuna ‘vimitihani’ vidogovidogo vingi huwa wapendanao wanapitia lakini kwa namna moja au nyingine wanakuwa wakivipotezea. Mtu anaamini mpenzi wake ni rahisi kubadilika mbele ya safari hivyo kumpa nafasi ya kuzidi kushibana.
Wengine kutokana na kuzidiwa na nguvu ya mapenzi, hawana muda wa kuangalia hivyo vimitihani. Wanaongozwa na matamanio. Wengine wanaongozwa na tamaa ya vitu kama fedha na mambo mengine.
Wanavifuga vimitihani kwa muda mrefu katika kipindi cha uchumba pasipo kujua ni jipu. Hawafikirii kabisa kwamba vimitihani hivyo vinaweza kuwa na madhara makubwa sana vitakakuwa jipu na kutumbuka wakati wakiwa tayari wameyaanza maisha ya ndoa.
Hapa nazungumzia zaidi tabia, nidhamu, uvumilivu na hulka mbalimbali. Japo kuna vitu mtu anaweza kuvificha katika wakati wa uchumba lakini Waswahili wanasema nyota njema huonekana asubuhi. Ni rahisi sana kumjua mtu kama anafaa au hafai.
Kwenye safari ya uchumba, kama umeona mwenzako ana tatizo la ulevi uliopindukia. Akishalewa anakuwa mkorofi, anaweza kukushikia panga muda wowote, ‘rehearsal’ yako ni kumueleza madhara na kumpa muda wa kubadilika kisha umpime kama amebadilika au laa!
Usikubali kumuacha hivyo alivyo ukategemea aje kubadilika wakati tayari mmeshaingia kwenye ndoa. Akiingia ndiyo itakuwa balaa zaidi. Kama alikuwa kwenye uchumba alikuwa anakukosakosa kukukata, anaweza kuja kukukata kabisa mkiwa ndani ya ndoa. Hakikisha hulka hiyo unaitibu, ukishindwa usiendelee mbele.
Ukikubali kuingia kwenye ndoa katika hali hiyo, tegemea maumivu huko mbele ya safari. Kama mwenzako ni malaya, hatulii nyumbani, rehearsal yako ni suala la kumbadilisha aachane na hiyo tabia. Mueleze kwa kirefu madhara ya tabia hiyo na umpe muda wa kubadilika, asipofanya hivyo, achana naye mapema.
Mpime kuhusu uvumilivu. Kama anaweza kukupenda katika nyakati zote. Uwe kwenye shida au raha. Mpime katika nyakati ngumu. Ikiwezekana mtengenezee mazingira magumu, mpime kuhusu uwezo wake wa kukabiliana na magumu.
Kwenye kipindi kama hicho, watu huweza kukimbiana. Unapompa mazingira magumu, akayaona hayawezi ni rahisi kukukimbia. Atamfuata mwingine ambaye hana mazingira magumu. Akifanya hivyo utakuwa umeshapata jibu.
Nasema hayo kwa sababu uzoefu unaonesha. Wengi hukurupuka katika ndoa. Hawajiridhishi vya kutosha katika hatua za awali. Matokeo yake wanaishia kukutana na maumivu mbele ya safari. Hapo ndipo wanajuta, wanatamani kuzirudisha siku nyuma ili watengue ndoa lakini wanakuwa wamechelewa.
0 Comments