Header Ads Widget

Korea Kaskazini Yarusha Makombora Mawili Baharini

Korea Kaskazini Yarusha Makombora Mawili Baharini

Korea Kaskazini imerusha makombora mawili ya masafa mafupi kuelekea baharini, karibu na pwani yake ya mashariki, saa chache baada ya nyambizi ya Marekani yenye silaha za nyuklia kuwasili katika kisiwa cha Jeju.

Vyombo vya habari vya Korea Kusini na Japan vimeeleza e kuwa makombora hayo yalifyatuliwa Jumatatu na yaliruka umbali wa kilomita 400, kabla ya kuangukia katika Bahari ya Mashariki, ambayo pia inajulikana kama Bahari ya Japan, iliyoko kati ya Rasi ya Korea na Japan. Taarifa ya pamoja ya majeshi ya Korea Kusini na Japan imeeleza kuwa makombora hayo yalirushwa kutoka eneo la karibu na Pyongyang.

Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida amelaani tukio hilo, akisema Korea Kaskazini imekuwa ikirudia mara kwa mara kurusha makombora, ambapo ni kitishio kwa amani na utulivu sio tu wa Japan, lakini pia kanda yote ya jumuia ya kimataifa, na jambo hilo halikubaliki kabisa.
”Ufyatuaji wa makombora unakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Japan tunalaani na kupinga kitendo hicho. Tutaendelea kufanya kila tuwezalo kufuatilia na kushirikiana kiusalama kupitia muungano wa Japan, Marekani na Korea Kusini, kulinda amani na utulivu wa kikanda,” alisema Kishida wakati akizungumza Jumanne na waandishi habari mjini Tokyo.
Ikulu ya Marekani nayo imelaani hatua ya Korea Kaskazini kurusha makombora hayo, ikiwa ni mara ya tatu kufanya hivyo tangu wiki iliyopita. Hata hivyo, jeshi la Marekani limesema kwamba urushaji huo wa makombora haukuwa na kitisho kwa maafisa wa Marekani, au kwa washirika wa Marekani.

Makombora hayo yamerushwa huku kukiwa na mvutano mkubwa katika Rasi ya Korea wakati ambapo Korea Kusini na Marekani zinajaribu kuongeza ushirikiano wa kijeshi katika kukabiliana na vitisho vinavyoongezeka vya nyuklia vya Korea Kaskazini.

Post a Comment

0 Comments