Header Ads Widget

Kocha Julien Chevalier Atuma CV zake Yanga

Kocha Julien Chevalier Atuma CV zake YangaMfaransa, Julien Chevalier.

Kocha Mfaransa Julien Chevalier atuma CV zake kuomba kuwa kocha wa Yanga

SIKU chache baada ya Yanga kutangaza kufikia makubaliano ya kuachana na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, imebainika kwamba, kila kukicha idadi kubwa ya makocha imekuwa ikituma wasifu wao kuomba kurithi mikoba yake akiwemo Mfaransa, Julien Chevalier.

Nabi ambaye alijiunga na Yanga Aprili 2021, tayari amemaliza mkataba wa kuinoa timu hiyo akiiacha kwenye mafanikio makubwa ya kushinda mataji sita ya ndani ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports, yote hayo amebeba misimu miwili mfululizo, 2021/22 na 2022/23.

Mbali na hilo, pia Nabi msimu wa 2022/23 ameifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kushika nafasi ya pili, mabingwa wakiwa USM Alger ya Algeria.
Kocha Julien Chevalier Atuma CV zake Yanga

Uongozi wa Yanga tayari umeweka wazi kuwa mara baada ya Nabi kuondoka Yanga wapo katika mipango wa kuhakikisha wanampata mbadala wake sahihi mapema iwezekanavyo.

Chanzo chetu cha ndani kutoka Yanga, kimeliambia Gazeti la Spoti Xtra kuwa, moja kati ya makocha ambao wametuma CV zao ni pamoja na Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Julien Chevalier mwenye umri wa miaka 42 raia wa Ufaransa.

“Ni kweli zaidi ya makocha 1000 wameomba kazi ya kuifundisha Yanga na tayari wametuma CV zao, moja kati ya makocha ambao wametuma CV za kutaka kuifundisha Yanga ni pamoja na Kocha wa ASEC, Julien Chevalier.

“Yanga kwa sasa wapo katika mchakato wa kuona ni jinsi gani watampata kocha sahihi kwa ajili ya kukinoa kikosi chao msimu ujao kwa mafanikio kama alivyofanya Kocha Nabi,” kilisema chanzo hiko.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, aliliambia Spoti Xtra kuwa: “Ni kweli kuna zaidi ya makocha 1000 ambao wametuma CV zao kwa ajili ya kuhitaji kuifundisha Yanga msimu ujao, wapo makocha wakubwa, lakini tuwahakikishie Wanayanga lazima tumpate kocha bora na mzuri atakayekuja kuipa mafanikio Yanga.”

Ikumbukwe kuwa, Kocha Julien Chevalier, mkataba wake na ASEC Mimosas unatarajiwa kufikia tamati Juni 30, mwaka huu. Kocha huyo mtaalamu wa kufundisha soka la pasi nyingi, alimfundisha Stephane Aziz Ki kabla ya kiungo huyo kutua Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2022/23.

Post a Comment

0 Comments