Mshambuliaji wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Ranga Chivaviro.
INASEMEKAMANA kuwa, mshambuliaji wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Ranga Chivaviro, amekataa dau la randi milioni 3 ambazo ni sawa na shilingi 358,737,000 za Kitanzania asajiliwe na Klabu ya Al-Akhdar ya nchini Libya.Chivaviro anatajwa kumalizana na Yanga, baada ya kufikia makubaliano na mabosi wa timu hiyo, ambaye atakuja kuwa mbadala wa Mkongomani, Fiston Mayele anayetajwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Mshambuliaji huyo alikuwa ananyemelewa pia na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo nayo ilipeleka ofa nono ya kumtaka, lakini akaichomolea.
Mtandao mmoja wa michezo kutoka Afrika Kusini, umeripoti kuwa Al-Akhdar wameonesha nia kubwa ya kumsajili mshambuliaji huyo aliyekuwa anachuana na Mayele katika ufungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Mtandao huo ulisema kuwa mshambuliaji huyo amegomea kitita hicho cha fedha alichotengewa kutokana na yeye mwenyewe kuonesha nia kubwa ya kutua Yanga.
Nyota huyo atajiunga na Yanga kama mchezaji huru, mara baada ya mkataba wake kumalizika wa kuichezea Marumo Gallants ambayo imeushuka daraja kutoka Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, hivi karibuni alizungumzia ishu ya usajili kwa kusema: “Tunakaribia kumalizana na mmoja wa washambuliaji wakubwa wa nchini Afrika Kusini ambaye jina lake ni siri kwa sasa.”
0 Comments