Watu wanaodaiwa majambazi wamepora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 25 katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la Tazara, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea jana saa 4 asubuhi wakati gari hilo likiwa kwenye foleni ya magari eneo hilo la taa za Tazara.
Watu hao wameporwa katika eneo ambalo huwa askari doria wametanda, lakini wakikamata pikipiki zinazotokea eneo la Buguruni.
Aidha taa za Tazara yaliko makutano ya barabara kutokea Buguruni, Temeke, Kariakoo/Posta na Gongo la Mboto ndilo eneo lenye askari wengi wakiwemo wa usalama barabarani.
Wakati tukio likifanyika kulikuwepo askari wenye magwanda maalumu ya askari doria zaidi ya watano wakivurumushana na waendesha pikipiki upande wa Barabara ya Mandela kutokesa Buguruni. Hata hivyo imeelezwa kuwa watu hao waliokuwa wakipeleka benki hawakuwa na ulinzi kama inavyoshauriwa na Jeshi la Polisi.
Majambazi hao waliokuwa watatu, walipora fedha hizo katika gari ndogo aina ya Toyota Rav4 yenye namba za usajili T 455 DFN mali ya kampuni ya kutengeneza mabati ya Sun Share iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyejitambulisha kwa jina la Richard Charles.
Kwenye gari pia alikuwepo mfanyakazi mwingine wa kampuni hiyo, mwenye asili ya China, aliyetambulika kwa jina la Cheng Deng.
Kwa mujibu wa dereva wa gari hiyo, Charles, walikuwa wakizipeleka fedha hizo benki eneo la Quality Centre na ndipo walipovamiwa na watu hao wakiwa na pikipiki aina ya boxer wakati magari yakiwa kwenye foleni wakisubiri taa ziwaruhusu kupita kutoka barabara ya Mandela.
Charles alisema majambazi hao walimwamrisha kufungua mlango na kuwapatia begi la fedha lililokuwa limewekwa katika kiti cha nyuma huku wakimtishia kwa bastola kabla ya kuvunja kioo cha nyuma cha gari hilo na kubeba fedha hizo na kutokomea nazo.
“Kwa kweli hata sielewi mpaka sasa hivi kilichotokea. Walikuja watu wawili mmoja upande wangu mwingine wa bosi wangu wakinitishia kwa bastola nifungue mlango niwape begi la fedha. Ghafla mtu mwingine akavunja kioo cha nyuma kwa kutumia kitako cha bastola na kubeba begi la fedha na kutokomea” alisema Richard.
Askari wenye silaha walifika katika eneo la tukio dakika 20 baada ya tukio hilo wakaishia kuhoji. Hata hivyo askari mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake alilaumu tabia ya baadhi ya watu kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha pasipo kuomba ulinzi wa polisi jambo linalohatarisha usalama wao na mali zao.
“Kama walijua wanasafirisha kiasi kikubwa hicho cha fedha kwa nini wasingeomba hata ‘escort’ (kusindikizwa kwa ulinzi) ya polisi? Hili ni tatizo, hasa katika kipindi hiki kigumu cha upatikanaji wa fedha, watu wanatakiwa kuchukua tahadhari mapema.” alisema askari huyo.
Credit: Habari Leo
0 Comments