Uchaguzi wa kumpata Meya wa Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, umefanyika na hatimaye Diwani wa Kata ya Pemba Mnazi kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Maabadi Hoja amechaguliwa kuwa Meya wa kwanza.
Uchaguzi huo ulifanyika jana kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, Rahel Mhando, ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi, alisema mgombea huyo wa CCM ndiye aliyeshinda.
Washiriki wengine walitoka vyama vya CCM, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mhando alisema Hoja alipata kura tisa dhidi ya Celestine Maufi (CUF) aliyepata kura tano na kura moja iliharibika.
Pia, Mhando alisema katika uchaguzi huo, Amini Sambo ambaye ni Diwani wa Kata ya Kibada, pia kutoka CCM, alishinda nafasi ya Naibu Meya, akipata kura 10 dhidi ya Ernest Mafimbo wa CUF, aliyepata kura tano. “Tunashukuru uchaguzi umefanyika vizuri Kigamboni, sasa tumepata Meya na Naibu Meya,” alisema Mhando.
Uchaguzi wa Meya na Naibu wake kwa upande wa Kigamboni, umefanywa baada ya Wilaya ya Temeke kugawanywa na kuwa wilaya mbili za Temeke na Kigamboni.
Mhando alieleza kuwa uchaguzi huo ambao ni wa mara ya kwanza kwa halmashauri hiyo, ulifanyika kwa amani bila kuwapo na malalamiko.
0 Comments