Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kila mkoa unatakiwa kuunda Kamati ya Amani kama njia ya kudumisha amani na utulivu kwenye mikoa yote nchini.
Waziri Mkuu ametoa wito huo jana usiku (Jumatano, Juni 15, 2016) wakati akizungumza na viongozi wa dini wa mkoa wa Dodoma na baadhi ya wazee maarufu wa mkoa huo aliowaalika kwenye futari katika makazi yake mjini Dodoma.
Amesema anatambua kuwa mkoa wa Dodoma uko shwari kwa sababu ya mshikamano uliopo baina viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo. “Nimegundua kuwa siri kubwa ya mkoa wa Dodoma kuwa na utulivu ni kuwepo kwa kamati ya amani yenye viongozi mahiri, kwani sote tunatambua kuwa kazi ya viongozi wa dini ni kuwaimarisha watu kiroho,” alisema.
Waziri Mkuu alisema ziko nchi zinatamani kuwa kama Tanzania kwa sababu wao hawana uhakika wa kulala na kuamka salama asubuhi. “Pamoja na yote sisi tuna uhakika wa asilimia 99 kulala usiku na kuamka salama asubuhi, kwa sababu ya amani iliyopo,” alisema.
Hadi sasa mikoa ambayo imekwishaunda kamati za amani ni Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Dodoma, Arusha, Lindi, Mtwara, Tanga na Mbeya.
Akigusia suala la mauaji ya hivi karibuni, Waziri Mkuu alisema anawaomba Watanzania kila mmoja kwa imani yake akemee kwa nguvu matendo hayo kwa sababu yeye haamini kama yamefanywa na Watanzania ambao wamelelewa kwenye misingi ya dini.
“Siamini kama kuna mtoto aliyelelewa kwenye misingi ya Uislamu anaweza kuingia msikitini na kuwaua wenzake wakati wakimwomba Mungu. Na wala siamini kama kuna mtoto aliyelelewa na kukuzwa Kikristo anaweza kuingia kwenye nyumba ya ibada akakuta watu wanasali na kuamua kuwaua. Ninawaomba tukemee kwa nguvu zote tabia hii,” alisisitiza.
Aliwataka watanzania wote wawe na walinzi wa wenzao kwa sababu kila mmoja ana jukumu la kumlinda mwenzake. “Tusiachie majeshi kazi hii kwa sababu kila mmoja na jukumu la kwanza kujilinda yeye mwenyewe na kisha kumlinda jirani yake,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Ahmed Said alisema wanawaombea dua Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika kazi za kuleta maendeleo kwa Watanzania. “Pia tutaendelea kuiombea nchi yetu ili Mwenyezi Mungu azidishe amani yake na watu wake waishi kwa amani, upendo na utulivu,” aliongeza.
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Dk. John S. Malecela ambaye alikuwa miongoni mwa wazee maarufu walioalikwa kwenye futari hiyo aliwataka waalikwa wenzake waendelee kuwaombea viongozi wa kitaifa na kusisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuombea amani ya Tanzania ambayo imedumu kwa miaka mingi iendelee kuwepo.
Katika hatua nyingine, Askofu wa Kanisa la Mennonite Tanzania Dayosisi ya Kati, Askofu Amos Muhagachi, ambaye alipewa fursa ya kutoa salamu fupi kwenye hafla hiyo, alisema kwenye mkoa huo hakuna magomvi ya kidini kwa sababu viongozi wa dini zote wanashirikiana kwa karibu sana.
“Hapa Dodoma Maaskofu tunashirikiana vizuri na Masheikh. Hivi sasa, masheikh vijana na wachungaji vijana wameanza kuiga haya tunayofanya, na zaidi ya yote tunashirikiana pia kuwaombea Rais wetu, Makamu wa Rais pamoja na wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu,” alisema.
0 Comments