WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema sukari haitakuwa tatizo katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na wakuu wa mikoa wamepewa maelekezo kilo moja isizidi Sh 2,300.
Alisema hayo jana wakati wa mahojiano na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano uliofanyika Chuo cha Mipango mjini hapa.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hadi Mei 13, mwaka huu walikuwa wamepokea tani nyingine 35,000 za sukari na haitakuwa tatizo kwa kuwa tayari jitihada kuwa serikali imefanya katika kushughulikia suala hilo.
Pia alisema sukari nyingine tani 11,000 imeshatoka na inasambazwa na nyingine tani 20,000 iko tayari Tanzania na tani nyingine 35,000 zinakuja kabla ya Juni 30, mwaka huu.
Alisema sukari wameigawa kwa kanda kutokana na kanda kutofautiana kulingana na wingi wa watu kwa mujibu wa mgawo wa Bodi ya Sukari Tanzania wamepeleka maeneo yote.
“Niwasihi Waislamu wenzangu ambao wamefunga Ramadhani kwamba suala la sukari halitakuwa tatizo,” alisema.
“Mwito wangu kwa wafanyabiashara kuwa waaminifu na kutambua sukari ni mahitaji ya Watanzania wote.”
Alisema suala la bei wameangalia kule juu wanaponunua Brazil, Uarabuni na Malawi wameshaweka viwango vya bei ambavyo wakuu wa mikoa wataangalia sukari haitazidi Sh 2,300 kwa kilo ili Watanzania wote wamudu kununua.
Alitoa mwito kwa wafanyabiashara kuacha kuficha sukari kwani hayo ni mahitaji ya wananchi wote na hawana sababu ya kufanya hivyo.
Katika miezi ya karibuni, sukari ambayo ni moja ya bidhaa muhimu nchini, imepanda bei hadi kuuzwa kati ya Sh 2,500 hadi 3,000 kwa kilo kutoka Sh takriban 1,800, hali iliyosababisha serikali kuingilia kati kuwataka wafanyabiashara kuuza kilo moja kwa Sh 1,800 na kuagiza sukari kutoka nje ili kukabili upungufu uliopo.
0 Comments