Header Ads Widget

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Awakemea Wanafunzi wa Kike Wanaofanya Biashara ya Kuuza Miili Yao


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amekemea tabia chafu zinazofanywa na baadhi ya wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu nchini wanaodiriki kushiriki kujiuza miili yao katika mahoteli makubwa na majumba ya starehe na kuwataka kuacha tabia hiyo.


Makamu wa Rais alisema hayo katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo hicho Kikuu ya kuadhimisha siku ya wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe pamoja na Uzinduzi wa Kampeni za uchangiaji wa Ujenzi wa Bweni la wanachuo wa kike.


Alisema baadhi ya wanafunzi hao walidiriki kujiuza miili yao kwa ajili ya tamaa ya kupata vitu vya anasa zikiwemo simu zenye gharama kubwa, mavazi na vitu vingine jambo ambalo linafedhehesha jamii, wazazi na walezi wao.


Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi wa kike wanaosoma katika vyuo vikuu nchini kujikita katika elimu ili waweze kufanikiwa kwenye maisha yao ya baadaye.


“Vyuo vimeharibika kwa tamaa, sisi tulisoma hapa Mzumbe na tuliweza kuishi, lakini wanafunzi wa sasa mnaingiwa na tamaa ya mashindano ya mavazi utadhani mnagombea Umiss,” alisema Suluhu.


Aliongeza kuwa, “nimeambiwa hapa Morogoro wapo baadhi ya wanachuo wa kike wanakwenda kujiuza miili katika hoteli moja kubwa na kwenye majumba ya starehe kwa tamaa tu, mnataka kuwa na simu ya laki saba na mavazi ya gharama kubwa itawezekana wapi, mnatukwaza wazazi wenu.”


Aliwaonya wanavyuo wenye tabia hiyo ya kuuza milii yao kuacha mara moja, huku akisisitiza kuwa dunia ipo tu hivyo wasifukuzane nayo kwani mambo hayo watayakuta baada ya kumaliza masomo yao.


Makamu wa Rais alitoa mfano kwa kuwaambia wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, “ukitaka kushika nafasi kubwa kama hii ‘yangu’ ni lazima ufuatiliwe historia yako tangu chini ukiwa shule ya msingi sasa kwa hali hiyo watoto wetu mtakosa fursa za kuwa viongozi wa juu.”


Alisema mtoto wa kike anakuwa na safari ndefu zaidi yenye misukosuko mingi kuliko mtoto wa kiume anapokuwa akitafuta elimu.


Samia alisema katika hatua ya elimu ya juu hasa kwa wanawake imegubikwa na changamoto ambazo kama wanajamii wa Tanzania tunapaswa kuungana na serikali kuziondoa ili kumuwezesha mtoto wa kike kufika mbali kielimu.


Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa mabweni, ufinyu wa fedha za kukidhi mahitaji na mtazamo hasi wa walimu na wanafunzi wa kiume dhidi ya wanafunzi wa kike wanapokuwa vyuoni.


Katika hatua nyingine, alisema Serikali imeanza kutoa elimu bure kwa wanafunzi wote kuanzia shule za msingi hadi kidato cha nne na kwamba hatua hiyo imeongeza idadi ya wanafunzi wakiwemo wa kike.

Post a Comment

0 Comments