Header Ads Widget

Bajeti ya Magufuli 2016/17 Hadharani Leo....Macho na Masikio Yote Yaelekezwa Dodoma


TANZANIA kama zilivyo nchi nyingine za Afrika Mashariki, leo inawasilisha bungeni mjini Dodoma Bajeti ya Serikali ili Bunge liijadili na kuipitisha, ianze kutekelezwa katika mwaka mpya wa fedha 2016/17 unaoanza Julai mosi.


Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango anatarajiwa kuiwasilisha bajeti hiyo inayoelezwa kuwa na Sh trilioni saba zaidi ya ile iliyopitishwa na Bunge hilo mwaka jana, ambayo utekelezaji wake unaishia Juni 30, 2016.


Hii ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, ambaye ameeleza kuwa anataka kujenga Tanzania ya viwanda, ambayo nia ni kuifanya iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.


Tofauti na bajeti ya mwaka jana ya jumla ya Sh trilioni 22.495 zilizotengwa kutoka katika vyanzo vya ndani na nje, bajeti nzima ya mwaka huu kwa mujibu wa mapendekezo ya ukomo wa bajeti hiyo yaliyowasilishwa kwenye mkutano wa wabunge wote Dar es Salaam, Aprili 6, mwaka huu ni Sh trilioni 29.539.


Bajeti hiyo inayosubiriwa kwa hamu na Watanzania, inatajwa kutokana na vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ambavyo kutokana na mapendekezo hayo ya awali, serikali imepanga kutumia Sh trilioni 17.719 kwa matumizi ya kawaida na Sh trilioni 11.82 kwa matumizi ya maendeleo ambayo ni sawa na asilimia 40 ya mapato ya ndani.


Mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yaliainishwa katika mapendekezo hayo ya bajeti kuwa ni Sh trilioni 2.693 wakati mapato kutoka Halmashauri yakiwa ni Sh bilioni 665.4.


Bajeti hiyo ya mwaka mpya wa fedha inategemewa kujumuisha fungu kutoka kwa washirika wa maendeleo ambalo ni asilimia 12 tu ya bajeti yote sawa na Sh trilioni 3.600.


Miongoni mwa vipaumbele vinavyotajwa kuzingatiwa katika bajeti hiyo ambavyo Dk Mipango aliwahi kuviainisha ni pamoja na utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka huo mpya wa fedha kwa kipindi cha miaka mitano.


Vipaumbele vingine ni viwanda vya kukuza uchumi pamoja na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu na kuweka mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara. Lengo la serikali ni kuhakikisha uchumi unakua kwa asilimia mbili zaidi kufikia asilimia 7.2 badala ya asilimia saba iliyopo.


Inategemewa pia kuwa mkazo zaidi kwenye bajeti hiyo utawekwa katika kukamilisha miradi ya maendeleo inayoendelea, miradi mipya, kulipa madeni yaliyohakikiwa na utekelezaji wa maeneo yote ya vipaumbele yaliyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka wa fedha unaoisha.


Mchango wa washirika wa maendeleo katika bajeti hiyo unahusisha misaada na mikopo, inayojumuisha maendeleo, mifuko ya pamoja ya kisekta na kibajeti.


Katika bajeti inayosomwa leo, serikali imependekeza mikopo ya Sh trilioni 5.374 kutoka katika soko la ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani zilizoiva pamoja na mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ya pamoja na kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa.


Aidha, katika mapendekezo yake ya ukomo wa bajeti hiyo, Dk Mpango alisema serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 2.11 kutoka kwenye soko la nje kwa masharti ya kibiashara.


Matarajio ya ongezeko la makusanyo ya kodi ni kufikia asilimia 12.6 huku makusanyo ya ndani na Halmashauri yakitegemewa kufikia asilimia 14.8.


Tangu Aprili 22, mwaka huu, wizara mbalimbali ziliwasilisha makadirio ya mapato na matumizi yake kwa mwaka wa fedha 2016/17 zikianzia na Ofisi ya Waziri Mkuu na kumaliziwa na Wizara ya Fedha na Mipango iliyowasilisha makadirio yake Juni mosi, mwaka huu.


Kwa siku sita kuanzia Juni 2, mwaka huu, serikali kwa kushirikiana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilikuwa inafanya majumuisho kwa kuzingatia hoja zenye maslahi kwa Taifa zilizojitokeza wakati wa kujadili Bajeti za Wizara.


Zipo changamoto mbalimbali zilizoelezwa na wabunge katika mijadala hiyo ya Bajeti za Wizara ambazo inatarajiwa kuwa serikali itakuwa imezichukua na inaweza kuzifanyia marekebisho kupitia Bajeti Kuu leo.


Bajeti ya leo ambayo itasomwa saa 10 kamili jioni na kuoneshwa moja kwa moja katika televisheni nchini, itatanguliwa na Taarifa ya Hali ya Uchumi itakayosomwa na Dk Mpango leo asubuhi.


Kesho wabunge watapata fursa ya kusoma na kutafakari hotuba hizo mbili kabla ya Ijumaa kuanza mjadala wake ambao utadumu kwa siku saba hadi Juni 20, mwaka huu ambayo utahitimishwa kwa uamuzi wa kura.

Post a Comment

0 Comments