Header Ads Widget

Watumishi Wavaa Vimini, vipedo, t-shirt, Jeans Kufyekwa Mshahara


HALMASHAURI ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, imepiga marufuku watumishi wote wa halmashauri hiyo kuvaa mavazi ambayo hayana maadili katika sehemu za kazi na kwamba atakayebainika atarudishwa nyumbani na kukatwa mshahara wa siku husika.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Adriano Jungu wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Bomani wilayani Muheza juzi.
Alisema lazima mtumishi ahakikishe staha ya mavazi aliyovaa kabla hajaingia kazini katika ofisi yake na kwamba mtumishi atakayekiuka kuvaa mavazi ambayo hayaendani na maadili sehemu ya kazi atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Akieleza zaidi, Jungu alisema kuwa mavazi ambayo hayaruhusiwi kwa watumishi ndani ya halmashauri yake ni pamoja na fulana, suruali za jeans, vimini, vitop, Pedo, yeboyebo, kaptula (pensi) na kandambili kwa sababu kuvaa vyote hivyo ni kinyume cha maadili ya utumishi.
Alisema kuwa mtumishi yeyote katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kabla ya kuingia kazini lazima aangalie mavazi aliyovaa na kwamba sheria iko katika waraka wa utumishi wa umma namba 3 wa mwaka 2007 na lazima watumishi waheshimu waraka huo.
Jungu alisema mtumishi yeyote katika halmashauri ya Wilaya ya Muheza ambaye atakiuka sheria hiyo kwa kuvaa nguo za kihuni wakati wa kuingia kazini basi atarudishwa nyumbani na atakatwa mshahara wake wa siku hiyo.
Alisema kuwa lazima watumishi waheshimu sehemu ya kazi kwa kuvaa nguo za heshima ikiwamo wanawake na wanaume kwa kuwa ofisi hizo wanaingia watu wenye heshima ikiwamo wazee sasa haiwezekani mtumishi mwanamke anaingia ofisini na kimini kinachofika katika magoti na hivyo mapaja yake yanaonekana sasa anamtamanisha nani.
Jungu alisema kuwa kwa wanaume nao lazima wawe na nidhamu ya kuvaa mavazi ya heshima na siyo kuvaa mavazi ya jeanz mlegezo na flana zinazowabana ni marufuku kabisa katika halmashauri ya Muheza.
Alisema ataanza kupita kila ofisi Jumatatu Mei 30 asubuhi kwa ajili ya kuwakagua mavazi yao watumishi hao wakiwamo wanawake na wanaume ili kukomesha tabia kama hiyo ambayo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma hapa Tanzania.
Jungu alitoa onyo kwa kupiga marufuku watumishi kufika kazini wakiwa wamelewa na mtumishi akibanika amefanya hivyo na ushaidi upo atampeleka hospitali kupimwa na akibainika atamtumbua jipu hadharani kwani serikali ya awamu ya tano ni ya hapa kazi tu.

Post a Comment

0 Comments