Mbunge wa Urambo Mashariki, Magreth Sitta amekemea lugha za udhalilishaji zinazotolewa dhidi ya wabunge wa kike ikiwa ni pamoja na sakata la lugha ya maudhi dhidi ya wabunge wa viti maalum wa Chadema wiki iliyopita.
Akitoa hoja binafsi bungeni mjini Dodoma, Mama Sitta ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wanawake, amesema kuwa vitendo havikubaliki na ni kinyume cha katiba na kanuni za Bunge.
Alisema kuwa vitendo hivyo licha ya kuwa vinawadhalilisha wabunge wanawake, vinashusha heshima ya chombo hicho cha kutunga sheria. Aliongeza kuwa ingawa Naibu Spika aliagiza lugha zote za udhalilishaji dhidi ya wabunge wanawake kuondolewa kwenye kumbukumbu ya Bunge, vitendo hivyo havikubaliki na havipaswi kujirudia.
Wiki iliyopita, wabunge wanawake wa Chadema walitoka nje ya Bunge kupinga kauli aliyoitoa Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga kuwa wabunge wa viti maalum wa chama hicho hupata nafasi hiyo kwa kuitwa ‘baby’ (kuwa na uhusiano wa kimapenzi) na viongozi wa ngazi za juu wa chama.
0 Comments