Header Ads Widget

Mchakato wa kumkabidhi Rais Magufuli Uenyekiti wa CCM waanza



Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatarajiwa kukutana kesho mjini Dodoma.

Chanzo cha kuaminika kimedokeza kuwa pamoja na mambo mengine, kikao hicho kitajadili maandalizi ya mkutano mkuu maalumu, ambao unatarajiwa kufanyika Juni mjini hapa.

Kwamba katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ataachia ngazi na kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli kama utamaduni wa chama hicho ulivyo katika kukabidhiana kijiti cha uongozi.

Tangu wiki iliyopita vikao kadhaa vya Sekretarieti vimekuwa vikiendelea mjini hapa, vikiwahusisha watendaji wa juu wa CCM pamoja na makatibu wa idara husika ambao huteuliwa na mwenyekiti kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Kikao hicho cha kesho pia kinatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Magufuli, ambaye tayari yupo mjini hapa alipokuja kwa ajili ya sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi – Mei Mosi.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa nao wataungana na viongozi wa ngazi za juu wa CCM katika kikao hicho.

Katika kikao cha kesho, Kamati Kuu pia itajadili na kupitisha majina ya wajumbe 10 wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kutoka miongoni mwa wabunge wa CCM.

Habari kutoka ndani ya chama hicho zilieleza kuwa kikao hicho kitakuwa chini ya Mwenyekiti wake Kikwete, ambapo wabunge walioomba nafasi hizo, majina yao yatapelekwa kwa wabunge wa chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura.

“Wabunge wana nafasi 10 za NEC na unajua waliokuwa wajumbe walishapoteza sifa za kuwa wajumbe, hivyo kwa kawaida kila Bunge jipya linapochaguliwa ni lazima uchaguzi ufanyike.

“Pamoja na kupitia majina ya wabunge waliojaza fomu, pia CC itajadili majina ya wabunge walioomba nafasi ya katibu wa wabunge wa CCM ambapo kuna wajumbe zaidi ya watatu wamejaza fomu,” kilisema chanzo hicho.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, miongoni mwa wabunge wanaotajwa kuwania nafasi ya katibu wa wabunge wa CCM yumo Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda, ingawa wapo wabunge wengine ambao kwa pamoja watachujwa na kikao cha kesho.

Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM anayemaliza muda wake ni Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama.
 
mpekuzi blog

Post a Comment

0 Comments