Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Elimu (Duce), jijini Dar es Salaam, Bertha Mwarabu (23), ameuawa na mwanafunzi mwenzake kwa kuchomwa kisu kwenye titi na tumboni kwa kinachodaiwa ni kutokana na wivu wa mapenzi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Mark Kalunguyeye, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika hosteli za chuo hicho zilizopo Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Kamanda Kalunguyeye amemtaja mtuhumiwa wa mauaji hayo kuwa ni Masamba Musiba (27) ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho, ambacho ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema mauaji hayo yalitokea juzi saa 3:45 usiku baada ya Musiba kuingia chumbani kwa marehemu ambaye inadaiwa alikuwa mpenzi wake na kuanza kumshambulia kwa kisu.
Ameongeza kuwa baada ya marehemu kuanza kushambuliwa, alipiga kelele kuomba msaada na ndipo wanafunzi wenzake walipokwenda na kumkamata mtuhumiwa wakati akijaribu kukimbia.
Amesema kelele za marehemu, ndizo zilizowashtua wanafunzi wenzake.
Kamanda Kalunguyeye alifafanua kuwa marehemu alikimbizwa hospitali kupatiwa matibabu lakini alifia njiani.
Mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, amesema tukio la mauaji hayo ni la kwanza kutokea chuoni hapo.
Profesa Mukandala alisema tangu aanze kufanya kazi chuoni hapo kwa miaka mingi, hajawahi kushuhudia tukio la namna hiyo na kuongeza kuwa amesikitika kwa kuondokewa na mwananfunzi huyo.
0 Comments