Jumapili iliyomalizika ilitawaliwa na habari ya ajali aliyodaiwa kuipata muimbaji wa Tip Top Connection, Tundaman maeneo ya Makambako wakati wakitokea kwenye show mjini Njombe.
Gari hiyo ilihusisha gari ndogo aina ya Toyota Aurion iliyokuwa ikiendeshwa na Musa ‘Man Katuzo’ Katunzi aliyefariki kwenye ajali hiyo.
Taarifa za awali zilidai kuwa Tundaman alikuwa mmoja wa abiria waliokuwemo kwenye gari hiyo. Lakini sasa imekuja kubainika kuwa, Tundaman hakuwemo kwenye gari hilo, bali alikuwa kwenye gari aina ya Noah.
Tetesi hizo zilikuwa kubwa zaidi kutokana na jinsi gari ilivyoharibika baada ya ajali hiyo huku Tundaman akidaiwa kutopata jeraha lolote ukilinganisha ma majerehi wengine watatu.
Tundaman anasisitiza kuwa alikuwemo kwenye gari hilo kwa kudai kuwa walikuwemo abiria watano. Utata kuhusu kutokuwemo kwa Tundaman kwenye gari hiyo ulianza kusambaa Jumanne hii kwenye mitandao ya kijamii.
Mimi niliiona kupitia HR wa kituo cha redio cha Ebony FM, Luther Akyoo aliyeandika kwenye Facebook: “TUKATAE TAIFA KUJENGWA KWA UONGO UONGO. Tundaman hakuwemo katika ajali hii mbaya, kinachoendelea naweza kuita ni ule ujanja ujanja wa kutafuta “Kiki” kupitia njia ambazo sio sahihi,” aliandika.
“Tundaman alikuwepo katika Noah, na yeye ni mmoja wa watu waliofika katika eneo la ajali hii na kumkuta Dereva na mmiliki wa gari akiwa ameishatutoka. Narudia, TUNDAMAN HAKUWEPO KATIKA GARI HII, watengeneza story yake watengeneze vyema na upya. Sidhani kama ni sahihi kwa upotoshaji huu kuendelea, tusikubali kuwa sehemu ya jamii ya watu kupokea habari zisizokua na uchunguzi wa kina,” alisisitiza.
“Ukweli ni huo, huyu alipata ajali alikuwepo kwenye shoo yake, baadaye aliondoka mapema, Tundaman hata ofisi za radio ebony FM alifika na gari aina ya NOAH, sio hii inayosambazwa mitandaoni. Hii ilipata ajali na mtu mwingine, Tundaman alifika kwenye eneo la TUKIO kama SHUHUDA mwingine,” aliongeza.
Niliamua kufuatilia kwa ukaribu zaidi habari hiyo kwa kuongea na Dj wa Ebony FM aliyekuwa host wa show zao na aliyedai kuwa ni kweli Tundaman hakuwepo kwenye gari iliyopata ajali. Anadai kuwa Tunda alikuwa kwenye Noah pamoja na wasanii wa Khanga Moko, Dj Kman na dereva.
Kujiridhisha nilizungumza na Dj Kman aliyekuwa akizunguka na Tundaman ambaye hata hivyo alisisitiza kuwa Tundaman alikuwemo kwenye gari iliyopata ajali.
Kipindi cha XXL cha Clouds FM nacho kiliamua kufanya uchunguzi wake na awali kiliongea na Tundaman aliyeendelea kusisitiza kuwa alikuwemo kwenye gari hilo.
Kipindi hicho kilizungumza na Kaimu Kamanda Mkuu wa polisi Iringa, John Kauga. Kamanda Kauga amedai kuwa gari iliyopata ajali ilikuwa na abiria wanne ambapo mmoja alifariki. Pia aliwataja majeruhi waliokuwemo kwenye gari hilo na jina la Tundaman halikutajwa.
Kwa maelezo hayo kila mmoja anaweza kujiridhisha kuwa Tundaman hakuwemo kwenye gari hilo jambo linalowashangaza wengi na kuwafanya waulize nini hasa sababu ya Tundaman kusema uongo katika suala kubwa kama hili.
Mimi na wewe hatukuwepo kwenye tukio hili na hatuna mamlaka ya kuhukumu, lakini kwa maelezo hayo yanayozipa ukweli tetesi hizo, Tundaman amenishangaza sana. Kuna mambo mengi mno ya kutafutia umaarufu lakini sio kwa hili.
Inashangaza pale mtu anapokuwa na amani tu kupokea pole pomoni kwa kitu ambacho hakuhusika nacho. Ajali hii imepoteza maisha ya kijana aliyekuwa na mke na familia yake iliyokuwa ikimtegemea – huwezi kuweka mzaha. Si ustaarabu kulaghai katika suala serious kama hili.
0 Comments