Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyelazwa juzi katika Hospitali ya Hindul Mandal aliruhusiwa jana akisema amepona na anaweza hata kushiriki mashindano ya mbio hadi Kibaha.
Maalim Seif juzi alilazwa katika hospitali hiyo baada ya kuugua ghafla akiwa kwenye ndege akitokea Zanzibar kuja Dar es Salaam na aliondoka hospitalini hapo jana saa 12.30 jioni.
Akizungumza wa waandishi wa habari, makamu huyo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema madaktari wa hospitali hiyo wamemhudumia vizuri na alianza kupata nafuu baada ya saa tatu, tangu alipofikishwa hospitalini hapo
“Kama mnavyoniona niko ‘fit’, nimelala usingizi mzuri leo na hali yangu imerudi kama kawaida, naweza hata kufanya mashindano ya kukimbia,” alisema baada ya kuteremka kutoka ghorofa ya tatu alikolazwa hadi chini kwa lengo la kuwaeleza waandishi wa habari kuhusu afya yake.
Maalim Seif ambaye alikuwa akitembea kwa ukakamavu, alisema amejisikia faraja baada ya watu wengi kutaka kufahamu maendeleo ya afya yake.
“Watanzania na Wazanzibari waliopo ndani na nje ya nchi wameonyesha mahaba makubwa kwangu kwa namna wanavyoendelea kufuatilia afya yangu, ninawashukuru sana,” alisema.
Akisimulia namna alivyougua, Maalim Seif alisema hali yake ilianza kubadilika akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar akielekea Dar es Salaam.
“Nilitoka nyumbani jana (juzi) nikiwa mzima wa afya, baada ya kuugua ghafla uwanja wa ndege, niliamua kuendelea na safari kwa kusaidiwa na wasaidizi wangu. Tuliamua kuja Hindu Mandal kwa ajili ya vipimo na matibabu,” alisema.
Alisema madaktari waliamua alale hospitali hapo ili akupata uangalizi wa karibu.
Kuhusu safari yake ya India, alisema; “namshukuru Mungu nimerudi salama na Ijumaa iliyopita nikapata mapokezi makubwa Zanzibar. "
Daktari wa Maalim Seif, Dk Omar Suleiman alisema makamu huyo wa Rais, alipata kizunguzungu na madaktari walipomfanyia uchunguzi hawakuona ugonjwa wowote hivyo walisema kizunguzungu hicho kilitokana na uchovu.
“Kwa hiyo matibabu na kusafiri muda mrefu kutoka India hadi Zanzibar, alihitaji muda mrefu wa kupumzika, nadhani ndiyo maana amepata kizunguzungu,” alisema.
Kama ilivyo kawaida kwa viongozi mbalimbali kutembelea wenzao wanapokuwa hospitali, jana ilikuwa tofauti kwa Maalim Seif baada ya kutoonekana kiongozi yeyote wa Serikali ya Zanzibar wala wa Muungano.
Viongozi waliomtembea ni wa CUF, akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Ismail Jussa.
0 Comments