Mchezo wa kwanza wa fainali ya klabu Bingwa barani Afrika umechezwa usiku wa October 31 kwa kuzikutanisha timu za USM Alger ya Algeria dhidi ya klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, huu ni mchezo ambao umechezwa Algeria na ndio mchezo wa kwanza wa fainali hizo ambazo kwa kawaida huchezwa nyumbani na ugenini.
TP Mazembe ambayo ina historia nzuri na michuano hiyo tofauti na USM Alger ambayo ndio ilikuwa inashiriki fainali yake ya kwanza ya kihistoria. Kipindi cha kwanza dakika za mwanzoni TP Mazembe walikuwa wamezidiwa, wakati USM Alger walionekana kumiliki mpira hadi dakika ya 27 Rainford Kalaba alipoifungia TP Mazembe goli la kuongoza.
Mchezo ulizidi kuwa na presha kutokana na kukamia kiasi kwamba dakika ya 45 Rainford Kalaba akaoneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa USM Alger, TP Mazembe kipindi cha pili waliingia kwa kujiami zaidi ambapo pasi ya Thomas Ulimwengu kwenda kwa Mbwana Samatta ilionekana kuwa na madhara baada ya Samatta kufanyiwa faulo katika eneo la 18 na kupiga penati iliyozaa goli la pili dakika ya 79.
USM Alger walipata goli la kufutia machozi dakika ya 88 ya mchezo kupitia kwa Seguer, ikiwa ni dakika 21 zimepita toka mchezaji wa USM Alger Orfi aoneshwe kadi nyekundu kutokana na kosa la kushika mpira kwa makusudi katika eneo la hatari, hadi dakika 90 zinamalizika USM Alger 1-2 TP Mazembe, timu hizo zitarudiana tena November 8 Lubumbashi.
0 Comments