Kama Bado Hujajiunga Nasi,kupata habari na matukio kila dakika Bonyeza Hapa sasa!
Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), limeitaka serikali kupitisha adhabu ya kunyongwa kwa wale wanaohusika na mauaji ya Albino.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Amani Kimataifa ya Albino jana jijini Dar es Salaam, Rais wa Chama cha Albino Tanzania (Tas), Joseph Tona, alisema kauli hiyo imetokana na ongezeko la idadi ya mauaji dhidi yao.
Kadhalika, takwimu za kutoka mwaka 2006 zinaonyesha kuwa Albino 74 wameshauawa kikatili, huku 56 wakinusurika kifo, na kati yao 11 wameongezewa ulemavu mwingine wa kudumu.
“Tunaadhimisha siku ya amani Tanzania, lakini hatuna amani kabisa, wenzenu tunakatwa viungo na kuuawa kama kuku bila huruma, kingine cha ajabu makaburi 18 ya albino wenzetu yamefukuliwa na miili yao imetolewa, picha hii inaashiria nini?” alihoji Tona.
Alisema hofu hiyo imesababisha maziko yao kutokuwa na heshima kama wengine kutokana na baadhi ya familia kuwazika wapendwa wao kwa siri na wengine ndani ya nyumba, au kuweka zege nzito katika makaburi kuzuia ufukuaji wa miili yao.
Alisema licha ya serikali kuweka vikosi kazi katika kudhibiti mauaji hayo, bado haisaidii kitu kutokana na baadhi ya polisi na maofisa kuwa miongoni mwa vinara wa kupokea rushwa.
Kwa mujibu wa Tona, matukio zaidi ya 120 ni kesi za mauji ya albino, kati yake 11 ndiyo yaliyofikishwa Mahakama, ambapo kati ya hizo kesi tano tu zimeweza kutolewa hukumu hadi sasa.
Akitoa ushuhuda mmoja kati ya waathirika ambaye mikono yake miwili imekatwa, Mariam Stanford, mkazi wa Ngara, mkoani Kagera, aliwataka wauaji wa albino wanyongwe hadharani ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo.
“Japokuwa Tanzania inasifika ndani na nje kama kisiwa cha amani, tafsiri hiyo ni kinyume kwani ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa mauaji ya kikatili, hivyo mwito wangu kwa viongozi wa dini tumieni midomo yenu kupinga hali hii kwa sababu na sisi tumeumbwa na Mungu na tunastahili kuisha kama wengine,” alisema Miriam.
Mkurugenzi wa Shirika la Under The Same Sun, Vicky Ntetema, aliishauri serikali kupitia vikosi kazi vilivyochukua jukumu la kuchunguza mauaji na ukatwaji wa viungo kwa albino, kutangaza matokeo kwa umma ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Pia, iuelezee umma matokeo ya kura za siri zilizopigwa katika mikoa tangu mwaka 2009 hadi sasa zibainishwe wazi kwani nyingi zimeonyesha waganga wa jadi kutumiwa na na viongozi wa kubwa katika kuwania nyadhfa mbalimbali serikalini.
Kutokana na hofu hiyo, ameitaka serikali kurejea mkakati wa mwaka 2009 uliotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ili kupiga marufuku leseni za waganga wa kienyeji na wale wa jadi.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alizitaka taasisi zilizopewa jukumu la kusimamia vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya walemavu hususani albino kutekeleza majukumu waliyopewa kisheria kwa uadilifu mkubwa jamii ya Watanzania ione haki inatendeka ili kudumisha amani ya nchi.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments