Na Mahmoud Ahmad-Simiyu
WAFUGAJI wawili wa kabila la Kitaturu wa kijiji cha Rukale Kata ya Bukundi wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu wameuawa kwa kupigwa risasi na kisha kuporwa mifugo yao waliyokuwa wakichunga katika kijiji cha Kakesio wilaya ya Ngorongoro mkoa wa Arusha na wafugaji wanaodaiwa waVKabila la Wamasai.
Tukio hilo limetokea Agosti 15 mwaka huu majira ya saa 4:00 asubuhi wakati wafugaji hao wakiwa wanachunga mifugo yao ipatayo 40 katika eneo hilo ambalo liko mpakani mwa mikoa hiyo na limekuwa na mgogoro kwa muda mrefu.Akizungumza jana na Waandishi wa habari mjini Mwanhuzi wilayani Meatu,Diwani wa Kata ya Bukundi,Joseph Masibuka alisema kuwa waliouawa ni wafugaji walioko katika eneo lake la utawala ambao ni wanaume na aliwataja kwa majina ya mwanzo kuwa ni Ruida na Rewita ambao wote wanakadriwa kuwa na umri wa miaka 35.
Alisema kuwa mara baada ya wafugaji hao kuuawa wenzao walipata taarifa na kuanza kufuatilia mifugo hiyo ambayo ilikuwa eneo la wilaya ya Ngorongoro na hapo mapigano yalipoanza kwa kutumia silaha za jadi na inasemekana katika mapigano hayo mfugaji mmoja wa kabila la Wamasai aliuawa.
Aliendelea kueleza kuwa taarifa hizo zilitumwa katika kituo cha polisi cha wilaya ya Meatu na ndipo askari polisi walifika eneo la tukio wakikutana na askari polisi wenzao kutoka wilaya ya Ngorongoro na kutuliza mapigano hayo huku wakiendelea kutafuta mifugo hiyo iliyoibiwa na walioshiriki mauaji hayo kwa kutumia risasi za moto.
Diwani huyo aliitaka serikali kuupatia ufumbuzi wa mgogoro huo wa kugombea eneo la malisho kati ya wafugaji wa maeneo hayo kwani umekuwa ni wa muda mrefu na bado haujapatiwa ufumbuzi.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Meatu,Dk Shali Shaku alikiri kupokea miili ya wafugaji hao waliouawa na walichukua jukumu la kuwazika baada ya ndugu zao kutofika kuuichukua miili hiyo.
‘Ni kweli tulipokea miili ya wafugaji hao wa kabila la Wataturu iliyoletwa na askari polisi tumeihifadhi hapa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa muda wa siku tatu na ndugu zao hawakuweza kufikia kuzichukua kwa kuwa zilikuwa zimeharibika vibaya tumeaamua kuizika jana”Alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu,Charles Mkumbo alisema kuwa kimamlaka hawezi kulizungumzia suala hilo kwani limetokea ndani ya Mkoa wa Arusha na hivyo kumwomba Mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha.
Hata hivyo juhudi za kumpata Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha,Liberatus Sabas hazikuzaa matunda kwani simu yake ilikuwa ikiitwa bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi hakujibu.
0 Comments