Wasichana 63 waliotekwa na kundi la Boko Haram mwezi mmoja uliopita wamefanikiwa kutoroka kutoka kwenye kambi waliyokuwa wamefichwa na kurejea makwao.
Kwa mujibu wa maafisa wa Nigeria, idadi hiyo inawajumuisha wanawake waliotekwa na Boko Haram kutoka kwenye kijiji cha Kummabza, Borno wiki mbili zilizopita.
Ingawa serikali kuu haikutoa taarifa rasmi juu ya tukio hilo, Gavana wa Borno, Alhaji Kashim Shittima alitoa maelezo juu ya taarifa hizo.
Vyanzo vya ulinzi, wakazi wa maeneo hayo na watu waliowashuhudia wanawake hao wamewaambia waandishi wa habari kuwa waliwashuhudia wanawake zaidi ya 60 waliorejea makwao Jumamosi.
Inaelezwa kuwa wanawake hao walitoroka Ijumaa usiku, wakati ambapo wanajeshi wa Boko Haram walienda kushambulia kambi za jeshi la Nigeria ambapo maafisa wanadai waliwauwa wanajeshi wa Boko Haram zaidi ya 50 katika mashambulizi hayo.
Hata hivyo, bado Boko Haram wanawashikilia wasichana wengine zaidi ya 200 waliowateka kati ya April na July mwaka huu.
0 Comments