Mpango wa kuligawa Shirika la Umeme (Tanesco) kuwa mashirika mawili umeiva, baada ya Serikali kupitisha Mkakati na Mwelekeo wa Sekta Ndogo ya Umeme (ESI).
Mpango huo utekelezaji wake unaanza Agosti mwaka huu, na lengo lake ni kuhakikisha uzalishaji wa umeme, unaongezeka kutoka megawati 1,583 zinazozalishwa kwa sasa hadi kufikia uzalishaji wa megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Ugawanyaji wa Tanesco maandalizi yake yanaanza Julai mwaka huu na utekelezaji wake utatimia Desemba 2017, ambako kutaanzishwa mashirika mawili.
Shirika moja litakuwa linashughulikia uzalishaji wa umeme na lingine litakuwa la kushughulika na usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Lengo kubwa la kugawanywa kwa Tanesco ni kuhakikisha Watanzania wanakuwa na uhakika wa kupatikana kwa nishati ya umeme kwa bei rahisi, ikiwa ni pamoja na kukuza pato la mtu mmoja mmoja.
Habari zilizopatikana jana, zinasema mwishoni mwa wiki Baraza la Mawaziri limebariki mkakati huo ;na sasa kilichobaki ni kwa Wizara ya Nishati na Madini, kuutangazia umma juu ya kuwepo mpango huo, unaotekelezwa chini ya mpango ujulikanao kama Electricity Supply Industriy (ESI).
Ili kukamilisha mpango huo, Serikali kwa sasa iko kwenye maandalizi kuhakikisha kuwa mpango huo kuligawanya shirika hilo unatekelezwa mwaka 2017, Tanesco haitakuwa na madeni yoyote.
Kwa kuanzia mwaka huu, Wizara ya Nishati na Madini imetenga Sh bilioni 565,71 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo, ikiwa ni pamoja na kulipa madeni ya Tanesco ambayo Serikali inadaiwa.
Lengo la mkakati huo, ambao unaihusisha Serikali, sekta binafsi, Tanesco, Ewura na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) ni kuinua pato halisi la Mtanzania kutoka pato la dola za Marekani 640 la sasa hadi kufikia pato la dola za Marekani 3,000 kwa mtu ifikapo mwaka huo.
"Tumekuwa tunafanya vizuri kwenye sekta ya umeme, lakini tunaamini tukitekeleza kikamilifu mkakati huu sekta ya umeme itachangia ukuaji wa pato la taifa na pato la mtu mmoja mmoja," alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi wakati akizungumza na mwandishi jana.
Chini ya mkakati huo, idadi ya watu waliounganishwa na umeme itaongezeka kutoka asilimia 24 ya sasa hadi kufikia asilimia 50, huku idadi ya wananchi wanaopata huduma ya umeme, pia itaongezeka kutoka asilimia 34 ya sasa hadi kufikia asilimia 75 mwaka 2025.
Maswi alisema mkakati huo utatekelezwa chini ya Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 na Sera ya Nishati ya mwaka 2003, ambazo zinatoa fursa ya Serikali kuvutia wawekezaji binafsi kushiriki katika kuzalisha umeme.
Lakini, pia mkakati huo unalenga kupunguza Serikali kugharimia uzalishaji wa umeme, badala yake sekta yenyewe ya umeme, ndiyo itakayokuwa inatoa gawio kwa Serikali, kama ilivyo kwa nchi nyingine, kama vile Thailand.
Mkakati huo pia unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme ; na kuhakikisha kuwa mahitaji ya umeme nchini na kwenye viwanda, yanatimizwa na wazalishaji wa sekta hiyo ya umeme.
Ili kutekeleza mkakati huo, Serikali imegawa utekelezaji wake katika hatua nne. Mkakati wa kwanza ni kuanzia Julai 2014 hadi Juni 2015, mkakati wa pili Julai 2015 hadi Juni 2018, awamu ya tatu itaanza Julai 2018 hadi Juni 2021 wakati awamu ya nne, ambayo ni ya mwisho utekelezaji wake utaanza Julai 2021 hadi Juni 2025.
Katika awamu ya kwanza, baadhi ya shughuli zitakazofanyika ni kuunda timu maalumu ya wataalamu kutekeleza mpango huo, kupitia upya Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 na kutekeleza mfumo wa kupunguza mfumo wa hasara kutoka asilimia 19 hadi asilimia 18.
Pia, wataboresha mifumo itakayotumika kwenye gridi ya Taifa wakati Tanesco itakapogawanywa. Pia, kutafanyika tathmini za masoko, uwezo wa rasilimali watu na uanzishwaji wa mfumo wa masoko ya umeme.
Katika awamu ya pili ni kupunguza mifumo ya hasara kutoka asilimia 18 hadi 16, kuigawa Tanesco kuwa na mashirika mawili na kupunguza utendaji wa Tanesco kutoka makao makuu na kuzipa ofisi za kanda mamlaka zaidi kabla ya mganyiko kufanyika.
Kwenye awamu ya tatu shirika la uzalishaji wa umeme, litafanya tathmini kwenye ofisi zake za kanda, kuweka mfumo wa uuzaji wa umeme kwa bei ya rejareja huku kampuni mbili zitakazokuwa zimeundwa, zitapewa jukumu la kuhakikisha mifumo ya hasara inapungua kutoka asilimia 16 hadi 14.
Katika awamu ya nne, Ewura itatakiwa iandae viwango vya uzalishaji wa umeme katika sekta ndogo ya umeme, kupunguza mifumo ya hasara hadi asilimia 12 na kuhakikisha asilimia 50 ya watu wanakuwa wameunganishiwa umeme; huku watumiaji wa nishati hiyo wanafikia asilimia 75 kupitia shirika la usambazaji pamoja na REA.
Kuwepo kwa ya Sheria ya Umeme na Sera ya Nishati ambazo zinatoa fursa ya kuanzishwa kwa Sekta Ndogo ya Umeme (ESI).
Kuwepo kwa mpango wa fedha ambao hadi kufikia mwaka 2017 mahitaji ya fedha katika sekta ya umeme, itakuwa ni dola za Marekani bilioni 11.4, kiasi ambacho ni sawa na dola za Marekani bilioni 1.9 kwa mwaka zinahitajika kutekeleza mpango huo.
Nchi kujiwekea malengo kuwa idadi ya watu watakaounganishwa ifikapo mwaka 2015 asilimia 30, asilimia 50 ifikapo mwaka 2025 huku itakapofika mwaka 2033 asilimia 75 ya Watanzania watakuwa wameunganishwa na umeme.
Kwa hali hiyo mkakati huo unafanya Tanesco igawanywe na kuwa mashirika mawili ili kukidhi mahitaji halisi ya nishati ya umeme.
Kutoa fursa kwa sekta ndogo ya umeme kuchangia maendeleo kwenye dira ya taifa ya mwaka 2025, kuhamasisha upatikanaji wa fedha na biashara katika sekta hiyo, upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa bei nafuu.
Utekelezaji wa mkakati huo, utapata nguvu zaidi baada ya kukamilika kwa bomba la gesi pamoja na ujenzi wa vinu vya kuzalisha umeme wa gesi asilia, hali itakayofanya Watanzania kupata huduma ya nishati ya umeme kwa bei rahisi
CREDIT: http://www.bongoclantz.com
0 Comments