Wakati wafanyabiashara wakiendelea kupuuza bei elekezi ya sukari iliyotolewa na Bodi ya Sukari (SBT), bidhaa hiyo imeanza kuadimika nchini. Bei elekezi ya sukari iliyotangazwa na serikali ni 1800.
Machi 8, Mkurugenzi Mkuu wa SBT, Henry Simwanza alitangaza kushusha bei ya sukari kutoka Sh2,000 hadi Sh1,800 akisema kiwango kilichopo cha bidhaa hiyo ni cha kuridhisha licha ya baadhi ya viwanda kusimamisha uzalishaji kutokana na msimu wa uvunaji mali ghafi kuisha.
Uchunguzi uliofanywa katika sehemu mbalimbali umebaini kuwa sukari haipatikani hata katika maduka makubwa (supermarket).
Kwa maeneo ambayo bidhaa hiyo inapatikana ilikuwa inauzwa kwa bei kubwa kuanzia Sh2,500 hadi 3,000 kwa kilo.Katika Mkoa wa Kilimanjaro, sukari imepanda kutoka Sh2,000 hadi Sh2,500.
Mkazi wa mjini Moshi, Joshua Temu alisema: “Maisha ya Watanzania wengi ni wale wa hali ya chini na mfumuko wa bei ya sukari huliumiza kundi hilo kutokana na uwezo mdogo wa kumudu gharama.”
Mfanyabiashara wa Soko la Mwananyamala, Issa Nduki alisema sukari haipatikani katika maduka ya jumla ndiyo maana hata upatikanaji wake sokoni unakuwa mgumu.Alisema hata ikipatikana huuzwa kwa bei ya juu kuanzia Sh120,000 hadi Sh130,000 kwa mfuko wa kilo 50.
Pia,gazeti la Mwananchi lilizunguka maeneo ya Kinondoni, Temeke na Ilala na kubaini kulikuwa hakuna sukari.Akizungumzia kuadimika kwa sukari, Ofisa Habari wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Edward Nkomola alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo kwani tayari wamelikabidhi mikononi mwa Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa.
Akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake bungeni mwishoni mwa Aprili, Majaliwa aliwataka Watanzania kuwa wavumilivu kwani Serikali tayari imeagiza sukari tani 100,000 kutoka nje kufidia uhaba uliopo na pindi itakapofika itauzwa kwa bei elekezi.
0 Comments