CHAMA Cha ACT-Wazalendo, jana kiliwasilisha rasmi hesabu zake katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hatua hiyo inatokana na agizo lililotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, la kuvitaka vyama ambavyo havijawasilisha hesabu kwa CAG, kutekeleza jambo hilo ndani miezi mitatu, kuanzia Aprili 27, mwaka huu.
Akizumgumza jana jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasilisha hesabu hizo, Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis, alisema mfumo wa chama hicho ni wa uwazi hali inayowafanya watekeleze na kuweka hadharani kila baada ya miezi mitatu.
“Baada ya kuwasilisha hesabu zetu katika ofisi ya msajili, tulipata barua iliyotuelekeza tupeleke hesabu zetu kwa CAG na wakati huo tulikuwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa marudio katika baadhi ya majimbo, hali iliyotufanya tushindwe kutekeleza agizo hilo,” alisema Khamis.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mitungi, katika barua yake ya Aprili 27, mwaka huu, kwenda ACT-Wazalendo, aliwaeleza kuwa baada ya miezi mitatu kupita bila chama hicho kuwasilisha hesabu zake kwa CAG, watatakiwa kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria.
Katika taarifa ya CAG iliyosomwa bungeni hivi karibuni ni chama kimoja pekee kilichotajwa kupeleka hesabu zake katika ofisi ya CAG.
Katika hatua nyingine, chama hicho kesho kinatarajia kuadhimisha miaka miwili, tangu kipate usajili wa kudumu, Mkuranga mkoani Pwani.
0 Comments